Ikiwa hukubaliani na uamuzi wa IRB-RPD wa kutakaa ombi lako, unaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo. Kukata rufaa sio tu nafasi ya pili ya kuwasilisha dai lako, lazima kuwe kuna makosa. Ukikata rufaa, utahitaji kuonyesha kwamba IRB-RPD ilifanya makosa katika uamuzi wao.
Soma barua ya Taarifa ya Uamuzi kwa makini, itaeleza sababu zilizofanya ombi lako likakataliwa. Unaweza pia kuomba upewe rekodi ya kesi yako ikiwa unataka kuisikiliza ili ikusaidie kuandaa rufaa yako.
Anayestahiki kukata rufaa
Wadai wa ukimbizi wengi wanaweza kukata rufaa (kuomba ombi lao lipitiwe) kwa IRB-RAD ikiwa dai lao la ukimbizi limekataliwa na IRB-RPD. IRB-RAD itakuambia ikiwa unaweza kukata rufaa.
Huenda usiweze kukata rufaa kwa IRB-RAD ikiwa:
- Uliondoa dai lako au ulitelekeza dai lako la ukimbizi.
- Uamuzi wa kukataa ombi lako wa IRB-RPD unasema kuwa dai lako halina msingi wa kuaminika au si la kweli.
- Uliingia Kanada kupitia mpaka wa nchi ya Marekani kwa kutumia mojawapo ya vighairi chini ya Makubaliano ya Nchi ya Tatu Salama.
- Wewe ni raia wa kigeni aliyeteuliwa.
- IRB-RPD ilikupa ulinzi wa wakimbizi halafu ikauondoa
Ikiwa huruhusiwi kukata rufaa kwa IRB-RAD, unaweza kuwasilisha ombi la Uhakiki wa Mahakama kwa Mahakama ya Shirikisho la Kanada ili wakague dai lako. Muulize wakili ni hatua gani unapaswa kuchukua.
Anza Taarifa yako ya Kukata Rufaa
Ili kuanza mchakato wa kukata rufaa, lazima:
- Ujaze fomu yako ya Taarifa ya Kukata Rufaa.
- Wataje watu wote unaowafanyia rufaa au kila mtu umfanyie Taarifa yake tofauti ya Kukata Rufaa.
- Tuma nakala tatu za Taarifa yako ya Kukata Rufaa kwenye barua au barua pepe kwa ofisi ya usajili ya IRB-RAD.
Ikiwa una mwakilishi wa kisheria anaweza kukusaidia kuwasilisha Taarifa ya Kukata Rufaa.
Baada ya kutuma fomu ya Taarifa ya Kukata Rufaa, utapokea Barua ya Kukiri kupokea ombi lako. Barua hii itakuambia tarehe ambayo lazima uwasilishe sehemu inayofuata ya rufaa yako, inayoitwa Rekodi ya Mkata rufaa. Pia itakujulisha ofisi ya usajili ya IRB-RAD utakapoituma, pamoja na maelezo ya mawasiliano ya hiyo ofisi, na pia itakueleza kitakachofuata.
Kamilisha rekodi yako ya Mkata rufaa
Rekodi ya Mkata rufaa ni sehemu muhimu ya rufaa yako. Katika Rekodi yako ya Mkata rufaa utaeleza kwa nini hukubaliani na uamuzi wa IRB-RPD. Hii ni nafasi yako ya kuonyesha makosa unayofikiri yalifanywa katika uamuzi huo.
Kwenye rekodi yako ya mkata rufaa, lazima:
- Ujaze fomu ya Rekodi ya Mkata rufaa.
- Fuata maagizo katika Mwongozo wa Anaekata Rufaa ujue hati na taarifa ambazo ni lazima uzieke kwenye Rekodi yako ya Mkata rufaa.
- Tuma hati zifuatazo, katika mpangilio huu:
- Nakala inayosimulia mkutano wa IRB-RPD wa kusikiza dai lako. Nakala hii si lazima uitume, utaituma ikiwa waona ukiituma itasaidia rufaa yako. Iwapo ungependa kuituma hii nakala, wewe au mwakilishi wako wa kisheria mtagharamika ili iandikwe kutokana na rekodi ya sauti ya mkutano wako. Utahitajika kuandika taarifa ya kuhakikisha kwamba nakala unayoituma haina hitilafu yoyote na lazima itiwe sahihi na mtu aliyeitengeneza.
- Ushahidi wowote ambao haukuruhusiwa na IRB-RPD wakati wa kusikilizwa kwa ombi lako la ukimbizi, au baada ya kusikilizwa kwa ombi lako la ukimbizi.
- Taarifa iliyoandikwa inayosema:
- Ikiwa unajumuisha ushahidi mpya ambao haukuwepo au haukupatikana wakati dai lako lilipokataliwa,
- Kama ungependa ombi lako lisikilizwe na IRB-RAD, na
- Kama utahitaji mkalimani awepo katika mkutano wa kusikiza ombi lako.
- Hati nyingine zozote zitakazosaidia rufaa yako.
- Sheria yoyote, sheria ya kesi, au hati nyingine za kisheria zinazosaidia rufaa yako.
- Hati ya kumbukumbu inayoelezea:
- Makosa yaliyofanywa na IRB-RPD ambayo ungependa yakaguliwe na IRB-RAD.
- Mahali makosa haya yatapatikana katika hati ya IRB-RPD au katika rekodi ya sauti ya mkutano wa ombi lako au katika nakala inayosimulia mkutano wa kusikiliza ombi lako.
- Uamuzi ambao ungependa IRB-RAD ufanye.
- Angalia Orodha ya Hakiki ya Rufaa ya IRB-RAD kabla ya kutuma Rekodi yako ya Mkata rufaa
- Tuma Rekodi yako ya Mkata rufaa kwa IRB-RAD. Unaweza ukatuma chapa mbili za Rekodi hiyo kenye barua au utume nakala moja ya kidijitali ya pdf kupitia barua pepe.
Hakikisha unatuma hati zako za rufaa kwa ofisi ya usajili ya IRB-RAD inayofaa. Ikiwa huna uhakika, angalia anwani ya IRB-RAD iliyoko kwenye barua uliyotumiwa ya kukiri kupokelewa kwa rufaa yako.
Uamuzi wa IRB-RAD
Mwanachama wa IRB-RAD anapofanya uamuzi kuhusu rufaa yako anaweza:
- Kukataa rufaa yako,
- Kuamua kukupa ulinzi wa wakimbizi, au
- Kutuma dai lako kwa Mwanachama tofauti wa IRB-RPD ili ombi lako lisikilizwe upya.
IRB-RAD itakutumia uamuzi wao pamoja na sababu za uamuzi huo katika barua. Pia watatuma nakala ya uamuzi huo kwa IRCC na CBSA.
Ikiwa rufaa yako ya IRB-RAD itakubaliwa
Iwapo IRB-RAD itaamua kukubali rufaa yako, wewe utakuwa ni mtu anayelindwa na utaweza kutuma maombi ya ukazi wa kudumu.
Ikiwa rufaa yako ya IRB-RAD itakataliwa
Iwapo IRB-RAD itakataa rufaa yako, unaweza kutuma maombi kwa Mahakama ya Juu ya kukagua kesi ili wakague uamuzi wa IRB-RAD. Usipotuma rufaa kwa Mahakama ya Juu ndani ya siku 15 baada ya ombi lako kukataliwa, CBSA inaweza kujaribu kukuondoa Kanada. Ukituma ombi la Mapitio ya ombi lako kwa wakati unaofaa, si lazima uondoke Kanada.
Unaweza kutuma ombi la kubakia nchini Kanada kwa misingi ya ubinadamu na ya huruma.
