Ni muhimu kukusanya na kutuma ushahidi kuhusu dai lako la ukimbizi kwa IRB-RPD. Ushahidi unajumuisha habari yoyote inayoonyesha unasema ukweli kuhusu wewe ni nani, kile ambacho tayari kimekupata, na kile ambacho unahofu kingekupata iwapo ukirudi katika nchi yako. Inaweza kuwa nyaraka, barua, makala ya magazeti, ripoti za matibabu ya kimwili au kisaikolojia, picha, rekodi za sauti, au hata video.
Ushahidi humsaidia Mwanachama kuamini kilichokupata, na kuelewa hali ilivyo katika nchi yako na kwa nini huwezi kurudi.
Wakati wa kuanza kukusanya ushahidi
Kupata ushahidi huchukua muda, hasa ikiwa unajaribu kuupata kutoka nchi nyingine. Anza kukusanya ushahidi haraka iwezekanavyo. Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, muulize ni ushahidi gani unaweza kukusaidia, muoneshe ushahidi ulionao, na umwambie auangalie. Chukua hatua haraka.
Masharti ya kutafsiri
Ushahidi wote, pamoja na rekodi za sauti, lazima ziwe kwa Kiingereza au Kifaransa. Usitumie Google kutafsiri na usitafsiri hati mwenyewe. Mfasiri mtaalamu ni bora zaidi. Ikiwa unapata huduma za kliniki ya kutoa msaada wa kisheria, gharama ya tafsiri inaweza kugharamiwa kwa sehemu au kikamilifu na kliniki hiyo. Ikiwa huna uwezo wa kulipia tafsiri, unaweza kutafuta mtu unayemwamini ambaye anajua lugha yako vizuri akutafsirie hati zako kwa Kiingereza au Kifaransa.
Mtafsiri wako lazima atie sahihi tamko ambalo unapaswa kutuma kwa IRB-RPD pamoja na hati ambayo ameitafsiri. Tamko hilo lazima liwe na:
- jina la mtafsiri,
- lugha na lahaja (ikiwa ipo),
- taarifa kwamba tafsiri hiyo ni sahihi, na,
- saini ya mfasiri.
Ushahidi wa kuunga mkono ombi lako
Kuna aina nne za ushahidi ambao unaweza kukusanya ili kuunga mkono dai lako.
Ushahidi wa kuonesha wewe ni nani
Unahitaji ushahidi wa kitambulisho chako na uraia wako. Hii inaweza kuwa:
- pasipoti,
- kitambulisho cha taifa,
- cheti cha kuzaliwa,
- cheti cha ndoa
- hati za shule au cheti cha shule,
- leseni ya kuendesha gari,
- kitambulisho cha wanajeshi, au
- uanachama wa kitaaluma au wa kidini.
Ushahidi wa aina nyingine pia unaweza kusaidia. Muulize mwakilishi wako wa kisheria ni ushahidi gani unaweza kuhitaji ili kudhibitisha wewe ni nani.
Ushahidi kuhusu madai yako
Unahitaji ushahidi ambao utaonyesha kwamba:
- Hadithi yako na matukio yaliyoko kwenye simulizi yako ni ya kweli
- Kwa kweli unaogopa kurudi katika nchi yako
- Uko hatarini katika nchi yako
- Serikali yako haiwezi kukulinda
- Si jambo la busara au salama kwako kuishi katika jiji tofauti ndani ya nchi yako
Hapa kuna baadhi ya maswali ya kukusaidia kupata ushahidi wa kusaidia dai lako:
- Je, una picha, barua, video, barua pepe, maandishi, au hati nyingine zinazoonyesha matatizo uliyokuwa nayo?
- Je, ulienda polisi au kwa wakala wa serikali kupata usaidizi? Pata nakala ya ripoti ya polisi au uthibitisho wa ziara yako.
- Je, ulipata msaada wa matibabu? Pata nakala ya rekodi za hospitali au za daktari.
- Je, kuna nakala za habari au machapisho mtandaoni kuhusu watu au matukio yanayohusiana na dai lako?
- Je, kuna watu walioshuhudia kilichotokea kwako? Waambie waandike taarifa inayosimulia kilichotokea na wakutumie. Ikiwezekana, waambie wathibitishe kuwa walichosema ni kweli mbele ya mwanasheria au mthibitishaji wa umma. Pia, waombe nakala ya kitambulisho chao.
- Je, kuna watu ambao wamepitia matatizo kama yako? Waambie waandike taarifa inayosimulia kilichotokea na wakutumie. Ikiwezekana, waambie wathibitishe kuwa walichosema ni kweli mbele ya mwanasheria au mthibitishaji wa umma.
- Je, madai yako yanatokana na kundi lako la kidini au la kisiasa, au kundi lingine ambalo wewe ni mwanachama? Pata hati zinazoonyesha uanachama wako.
- Je, una matatizo ya ki akili kwa sababu ya kile kilichotokea? Pata ripoti kutoka kwa daktari, mwanasaikolojia, au mshauri wa afya ya akili nchini Kanada. Hii inachukua muda, kwa hivyo fanya hivi haraka uwezavyo.
- Je, uko kwenye mitandao ya kijamii? Piga picha za machapisho yoyote kwenye mtandao yanayohusiana na hadithi yako.
Huenda usiweze kupata ushahidi wote unaotaka kutoka nchi yako kwa sababu si salama kufanya hivyo, au kwa sababu ni vigumu sana kuupata. Jaribu uwezavyo ili upate ushahidi, na kama huwezi kupata ushahidi fulani, eleza kwa maandishi kwa IRB kwa nini hukuweza kuupata.
Ushahidi kuhusu hali ya nchi ilivyo
Unaweza kuwasilisha ushahidi unaoonyesha hali katika nchi yako ilivyo na jinsi yanavyohusiana na dai lako. Hii inajumuisha ripoti za kuaminika kuhusu hali ya kisiasa, kijamii, kitamaduni, kiuchumi na haki za binadamu katika nchi yako.
IRB-RPD huhifadhi hati za umma kuhusu hali ilivyo katika nchi zote ulimwenguni katika Vifurushi vya Nyaraka vya Kitaifa (NDPs).
Jihadhari! Baadhi ya hati katika NDP zinaweza kuwa ni za zamani. Huenda hali katika nchi yako imebadilika au uliyoyapitia huenda yasiwe katika NDP. Zungumza na mwakilishi wako wa kisheria ili kuona ni maelezo gani mapya yanaweza kusaidia dai lako.
Kwa mfano, unaweza kutuma:
- makala ya habari au video za hivi karibuni,
- taarifa kutoka kwa mashahidi wa kitaalamu,
- makala za kitaaluma, au
- ripoti za haki za binadamu.
Tazama Vifurushi vya Nyaraka vya Kitaifa za nchi yako.
Ushahidi kutoka kwa mashahidi
Unaweza kuwa na mashahidi katika kusikilizwa kwako watakaozungumza kuhusu madai yako. Shahidi ni mtu ambaye ana taarifa muhimu kuhusu wewe na dai lako. Wakati wa kusikilizwa kwako, mashahidi watajibu maswali kutoka kwa wakili wako na kutoka kwa Mwanachama. Mashahidi hawawezi kusikiliza unachosema wewe kwenye kesi na huwezi kuzungumza nao wakati wa mapumziko. Wakati mwingine Mwanachama anaweza asihitaji kuwauliza mashahidi wako wazungumze.
Ikiwa una shahidi, toa taarifa ifuatayo kwa maandishi kwa IRB-RPD, angalau siku kumi kabla ya tarehe yako ya kusikilizwa.
- Maelezo yao ya mawasiliano (anwani, nambari ya simu, na nambari ya faksi)
- Taarifa fupi ikieleza kwa nini wanahitaji kuzungumza
- Unadhani wataongea kwa mda gani
- Uhusiano wako nao
- Ikiwa watazungumza ana kwa ana, kupitia mkutano wa video wa mtandaoni, au kwa kutumia simu
- Ikiwa wanahitaji mkalimani, na lugha na lahaja wanayoongea
- Ikiwa shahidi ni mtaalam, habari kuhusu utaalamu wao, na ripoti fupi ya kile watakachosema, iliyosainiwa nao.
