Iwapo IRB-RPD itakubali dai lako la ukimbizi, wewe utakuwa Mkimbizi wa Mkataba au Mtu Aliyelindwa. Hii inamaanisha kuwa wewe (na familia yako iliyo ndani na nje ya Kanada) mnaweza kutuma ombi la ukazi wa kudumu. Ikiwa unaishi Quebec, utahitaji pia kutuma ombi ya Cheti cha Quebec cha Kuchaguliwa.
Je, nitafanya nini ikiwa Waziri atakata rufaa dhidi ya ombi langu?
Waziri anaweza kutaka uamuzi wa IRB-RPD wa dai lako upitiliwe. Hii ina maanisha kwamba Waziri amekata rufaa dhidi ya uamuzi wa ombi lako kukubaliwa. Ili Waziri aweze kukata rufaa, lazima aonyeshe kwamba IRB-RPD ilifanya makosa katika uamuzi wa dai lako la ukimbizi.
Ikiwa Waziri atakata rufaa ndani ya siku 15 ya ombi lako kukubaliwa, unapaswa kusimamisha ombi lako la makazi ya kudumu.
Ikiwa Waziri atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa ombi lako, utajulishwa na utapata fursa ya kujibu. Unapojibu, utahitajika utoe sababu za kueleza ni kwa nini hukubaliani na rufaa hiyo ya Waziri.
Ili kujibu rufaa, wewe au mwakilishi wako wa kisheria mtalazimika:
- Kutayarisha Taarifa ya Nia ya Kujibu Rufaa.
- Tayarisha Rekodi ya Mhojiwa inayoeleza sababu zinazofanya hukubaliani na rufaa pamoja na hati zozote za kukusaidia.
- Tuma nakala ya nyaraka hizi zote mbili kwa Waziri na kwa ofisi ya IRB-RAD katika eneo lako kupitia tovuti ya My Case. Ikiwa huna My Case, unaweza kuzituma kwa barua pepe au kwa posta. Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, anapaswa kufanya hivi kwa niaba yako.
- Toa uthibitisho kwa IRB-RAD kwamba umetuma hati zako kwa Waziri.
Baada ya kujibu rufaa kwa kutuma hati zinazohitajika, IRB-RAD kwa kawaida huwa itafanya uamuzi wao bila ya kufanya kikao cha kukusikiliza. Wakati mwengine, Waziri anaweza kusema kuwa ni lazima kesi isikilizwe tena.
IRB-RAD itafanya mojawapo ya maamuzi yafuatayo:
- Wanaweza kukubaliana na uamuzi wa IRB-RPD. Hii inamaanisha kuwa uamuzi wa kukubali ombi lako utabakia.
- Wasikubaliane na uamuzi wa IRB-RPD, na waubadilishe uamuzi huo.
- Kurejesha kesi yako kwa IRB-RPD ili kesi yako isikilizwe upya.
Kusafiri nje ya nchi ya Kanada
Ikiwa unapanga kusafiri nje ya nchi ya Kanada baada ya kupewa hadhi ya mkimbizi au kuwa mtu aliyelindwa, lazima utume ombi kwa ofisi ya Pasipoti ya Kanada ili upate Hati ya Wakimbizi ya Kusafiri. Ikiwa Waziri amekata rufaa dhidi ya ombi lako, usitoke nje ya nchi ya Kanada.
