Sheria Mpya nchini Kanada zinaweza kuathiri ustahiki wa dai lako la ukimbizi, hata kama tayari umewasilisha ombi lako. Baadhi ya taarifa kwenye tovuti hii zimepitwa na wakati. Tunazisasisha. Zungumza na wakili au mtoa huduma wa makazi unayemwamini. Jifunze Zaidi

Mchakato wa Madai ya Ukimbizi Wafafanuliwa

Mkimbizi ni nani?

Serikali ya Kanada inasema wewe ni mkimbizi ikiwa hauko salama katika nchi yako. Ukirudi nyumbani, unaweza kuumizwa au kupoteza uhuru wako kwa sababu ya kubaguliwa. Lazima uishi nchi nyengine.

Kuomba ulinzi wa mkimbizi nchini Kanada kunaitwa kufanya dai la ukimbizi. Hata kama ulitendewa vibaya katika nchi yako au nchi yako ni mahali pa hatari, huenda usiruhusiwe kukaa Kanada. Ni lazima uonyeshe kuwa wewe ni Mkimbizi kulingana na Mkataba wa Geneva au wewe ni Mtu Anayehitaji kulindwa.

Mkimbizi kulingana na Mkataba wa Geneva

Ili kuwa mkimbizi wa Mkataba wa Geneva, sentensi hizi sita lazima ziwe kweli kwako:

  • Nikirudi katika nchi yangu, kuna uwezekano nitatendewa vibaya sana.
  • Nitatendewa mabaya kwa sababu ya mimi ni nani au naamini nini
  • Kwa kweli naogopa kurudi.
  • Nina sababu nzuri ya kuogopa kuishi katika nchi yangu.
  • Serikali yangu haiwezi kunilinda.
  • Siwezi kuishi kwa usalama au kwa njia inayofaa katika sehemu nyingine yoyote nchini kwetu.

Mtu Anayehitaji Ulinzi

Ili kuwa “mtu anayehitaji ulinzi”, lazima uonyeshe kuwa 1 au 2 ni kweli:

1. Nikirudi katika nchi yangu, huenda watu walio na mamlaka watanitesa.

AU

2. Nikirudi katika nchi yangu, naweza kufa au kutendewa ukatili au kuadhibiwa,

NA

  • Serikali yangu haiwezi kunilinda,
  • Siwezi kuishi kwa usalama au kwa njia inayofaa katika sehemu nyingine yoyote nchini kwetu.
  • Niko hatarini lakini sio kila mtu katika nchi yangu ana hatari hii,
  • Siko hatarini kwa sababu tu nchi yangu inataka kuniadhibu kwa kufanya jambo ambalo ni uhalifu nchini Kanada, na
  • Siko hatarini kwa sababu tu ya huduma duni za afya katika nchi yangu.

Tazama Elewa Ufafanuzi wa Kisheria kwa maelezo zaidi.

Je, ninaweza kufanya dai la ukimbizi?

Serikali ya Kanada itaamua kama unaweza kufanya dai la ukimbizi. Ni muhimu kuelewa ni nani anayeweza kutoa dai. Pata ushauri wa kisheria kabla ya kuomba ulinzi wa wakimbizi.

Nani haruhusiwi

Huenda usiruhusiwe kufanya dai la ukimbizi nchini Kanada ikiwa:

  • Wewe ni mkimbizi wa Mkataba wa Geneva katika nchi nyingine ambayo unaweza kwenda.
  • Ulituma dai la ukimbizi nchini Marekani, Uingereza, Australia au New Zealand.
  • Tayari uliambiwa na Kanada kwamba huwezi kutoa dai la ukimbizi.
  • Uliwahi kutoa dai la ukimbizi nchini Kanada ambalo liliondolewa, liliachwa au lilikataliwa.
  • Umetambuliwa kuwa hatari au mhalifu, au umevunja sheria za haki za binadamu.
  • Tayari ulipewa hadhi nchini Kanada kama mtu anayelindwa.
  • Uliamriwa na serikali ya Kanada uondoke.
  • Katika mpaka wa nchi kavu wa Marekani na Kanada, hukuweza kuingia kwa sababu ya Makubaliano ya Nchi ya Tatu ya Salama (STCA).

Makubaliano ya Nchi ya Tatu ya Salama (STCA).

Ukiingia Kanada kutoka Marekani, makubaliano kati ya Kanada na Marekani yanayoitwa Mkataba wa Nchi ya Tatu ya Salama (STCA) hufanya iwe vigumu kuomba ulinzi wa wakimbizi. Mkataba unasema kwamba unapaswa kufanya madai yako ya ukimbizi katika nchi ya kwanza iliyo salama utakayoingia. STCA itatumika kwako ikiwa utaingia Kanada kwa kuvuka mpaka rasmi, au uliingia Kanada ukitumia kivuko rasmi cha mpaka na ukatoa dai la ukimbizi ndani ya siku 14 baada ya kuingia nchini.

Ukivuka hadi Kanada kutumia mpaka wa ardhi, unaweza tu kutoa dai la ukimbizi ikiwa:

  • Una familia nchini Kanada.
  • Wewe ni mtoto chini ya miaka 19, unasafiri peke yako, na huna mzazi au mlezi wa kisheria nchini Marekani.
  • Una visa halali ya Kanada, au kibali cha kusoma au cha kufanya kazi.
  • Unakabiliwa na hukumu ya kifo nchini Marekani au katika nchi yako.
  • Wewe huna taifa.
  • Wewe ni raia wa Marekani.

Afisa wa mpaka atakuuliza maswali ili kuona kama unastahiki mojawapo ya vighairi hivi. Ikiwa unastahiki, utaruhusiwa kuingia Kanada. Ikiwa hustahiki kwa sababu ya mojawapo ya vighairi, unaweza kurudishwa Marekani. Ikiwezekana, zungumza na wakili au mwakilishi wa kisheria kuhusu njia nyingine unazoweza kujaribu kubaki Kanada.

Tazama Makubaliano ya Nchi ya Tatu ya Salama kwa maelezo zaidi.

Muhtasari wa mchakato wa kudai ukimbizi

Ili kukaa Kanada, ni lazima uonyeshe serikali kwamba wewe ni mtu Kanada inamuita mkimbizi. Hii inamaanisha ni lazima uonyeshe kuwa wewe ni Mkimbizi kulingana na Mkataba wa Geneva au ni Mtu Anayehitaji Ulinzi. Ikiwa una hadhi ya usafiri katika nchi zaidi ya moja, lazima uonyeshe kuwa uko hatarini katika nchi zote hizo. Lazima pia uonyeshe kuwa unasema ukweli kuhusu wewe ni nani na hadithi yako ni ya kweli. Utafanya hivi kwa kukusanya ushahidi na kwa kuwa mwaminifu, mkweli, na ueleze kwa kina kuhusu kile kilichotokea kwako.

Anza dai lako la ukimbizi

Hatua ya kwanza katika kufanya dai la ukimbizi ni kuijulisha serikali ya Kanada kuwa unataka ulinzi. Kuna njia mbili za kufanya hivi. Lazima uwe Kanada.

  • Ikiwa uko ndani ya Kanada: kamilisha na utume ombi lako la mtandaoni kwenye tovuti ya IRCC, au
  • Ikiwa uko mpakani, kwenye uwanja wa ndege, au katika kituo cha kizuizini: mwambie afisa wa CBSA kwamba unataka kufanya dai la ukimbizi.

CBSA au IRCC wataamua kama unaruhusiwa kufanya dai la ukimbizi nchini Kanada. Ukiwa waruhusiwa, watatuma dai lako kwa IRB-RPD.

Tazama Anza Dai Lako la Ukimbizi kwa maelezo zaidi.

Usikilizaji wa dai lako la ukimbizi

Ombi lako la ukimbizi litasikizwa. Wakati wa kusikilizwa kwako, mtu kutoka IRB-RPD (Mwanachama) atasikiliza hadithi yako na mashahidi wako. Wataangalia Fomu yako ya BOC, maelezo kutoka IRCC au CBSA, na kitu kingine chochote ulichowapa.

Tazama Katika Kusikizwa kwa Ombi Lako la Wakimbizi  kwa maelezo zaidi.  

Baada ya Kusikizwa kwa Ombi Lako la Ukimbizi 

Baada ya kusikilizwa kwako, IRB-RPD itakuambia kama dai lako la mkimbizi limekubaliwa. Likikubaliwa, unaweza kutuma maombi ya kuwa mkazi wa kudumu. Dai lako likikataliwa, unaweza kukata rufaa (uombe ukaguzi wa ombi lako). Zungumza na wakili au mwakilishi wa kisheria ili upate kujua una chaguo gani.

Tazama Baada ya Kusikizwa kwa Ombi Lako la Wakimbizi kwa maelezo zaidi.


Sehemu inayofuata ya mwongozo: 1.2 Kutana na Wakala Tatu za Serikali