Ili dai lako la ukimbizi likubaliwe, ni lazima uonyeshe kuwa wewe ni Mkimbizi kulingana na Mkataba wa Geneva au Mtu Anayehitaji Ulinzi. Mwanachama wa IRB-RPD atafanya uamuzi baada ya kusoma hati zako na kusikiliza hadithi yako.
Unahitaji kuelewa ufafanuzi na jinsi ya kukusanya ushahidi ili kusaidia dai lako.
Soma kila sehemu ya ufafanuzi. Kwa kila sehemu ambayo ni kweli kwako, tengeneza orodha ya ushahidi unaoweza kupata ili kuonyesha kuwa ni kweli. Mpe mwakilishi wako wa kisheria orodha hiyo.
Mkimbizi kulingana na Mkataba wa Geneva
Ili kuwa mkimbizi wa Mkataba wa Geneva, sentensi hizi sita lazima ziwe kweli kwako:
- Nikirudi katika nchi yangu, kuna uwezekano nitakumbana na mateso (kutendewa vibaya sana).
- Ningeteswa kwa sababu ya rangi yangu, dini, utaifa, maoni ya kisiasa, au kwa sababu ya kikundi cha kijamii ninachotoka.
- Kwa kweli naogopa kurudi.
- Nina sababu nzuri ya kuogopa kuishi katika nchi yangu.
- Serikali yangu haiwezi kunilinda.
- Siwezi kuishi kwa usalama au kwa njia inayofaa katika sehemu nyingine yoyote nchini kwetu.
Mtu Anayehitaji Ulinzi
Ili kuwa mtu anayehitaji ulinzi, lazima uonyeshe kuwa 1 au 2 ni kweli:
- Nikirudi katika nchi yangu, huenda watu walio na mamlaka watanitesa. AU
- Nikirudi katika nchi yangu, naweza kufa au kupata mateso ya kikatili au kuadhibiwa, na…
- Serikali yangu haiwezi kunilinda,
- Siwezi kuishi kwa usalama au kwa njia inayofaa katika sehemu nyingine yoyote nchini kwetu.
- Niko hatarini lakini sio kila mtu katika nchi yangu ana hatari hii,
- Siko hatarini kwa sababu tu nchi yangu inataka kuniadhibu kwa kufanya jambo ambalo ni la uhalifu nchini Kanada, na
- Siko hatarini kwa sababu tu ya huduma duni za afya katika nchi yangu.
