Sehemu hii itakupa muhtasari wa jinsi dai la ukimbizi linavyoanza. Itajibu maswali ya msingi. Itakuelekeza jinsi ya kuanza dai lako.
Pata maelezo ya kina kuhusu jinsi ya kuanzisha dai lako la ukimbizi katika Sehemu ya 4 – Anza Dai Lako la Ukimbizi.
Maswali ya kawaida
Unaweza kuanza dai lako la ukimbizi wakati unawasili Kanada au ukiwa tayari uko Kanada. Unaweza kuwa na maswali mengi:
- Je, nitaanzaje dai langu la ukimbizi?
- Mchakato huu utachukua muda gani?
- Nini kitatokea ikiwa dai langu litakataliwa?
- Ni lini nitaunganishwa tena na familia yangu?
- Je, nitapataje msaada?
- Je, hadithi yangu itaaminika?
Usijali! Kuna watu wengi ambao wanaweza kukusaidia kwenye huu mchakato. Rudi kwenye tovuti hii wakati wowote ili upate msaada.
Pata usaidizi wa kisheria
Mchakato wa kudai ukimbizi unaweza kuwa mrefu na mgumu. Pata usaidizi wa kisheria haraka uwezavyo.
Pindi utakapoamua kufanya dai lako, pata usaidizi wa kisheria kujaza Fomu yako ya Msingi wa Madai (BOC). Itachukua muda kufanya kazi na mwakilishi wa kisheria ili kuweka mambo yote muhimu katika BOC yako.
Mwakilishi wa kisheria anaweza kukusaidia kujaza fomu na kutayarisha hati zote. Anaweza kwenda nawe kwenye kikao cha kusikilizwa kwa dai lako na kukusaidia kueleza hadithi yako.
Jua una chaguo gani
Fanya utafiti na upate ushauri wa kisheria kabla ya kuanza dai lako. Hakikisha kuwa kutuma dai la ukimbizi ndio chaguo bora kwako. Elewa jinsi uamuzi huu unaweza kuathiri maisha yako ya baadaye.
Makinika
Makinika na uchukue muda wako kujaza Fomu yako ya BOC. Fomu ya BOC ni muhimu sana na unaweza kulazimika kuizungumzia siku ya kusikilizwa kwa dai lako. BOC lazima ijumuishe matukio yote muhimu katika maisha yako ambayo yanaonyesha kuwa wewe ni mkimbizi.
Jijali
Kufanya madai ya ukimbizi ni kazi ngumu. Chukua mambo hatua moja baada ya nyingine. Kumbuka kujijali.
Kuwa makini
Utapokea karatasi na hati nyingi wakati wa mchakato wako wa dai la ukimbizi. Kuna faili iliyogawanywa sehemu tofauti ya kuweka hati zako na kuzipanga. Jaribu kupata moja, na uanze kuitumia.
Tengeneza nakala na uweke makaratasi yako vizuri.
Weka makaratasi na nyaraka zozote za serikali, hata kama muda wake umeisha. Huenda wewe au mwakilishi wako wa kisheria mtazihitaji.
Jitayarishe kwa mahojiano yako ya kuamua kama unastahiki kuwa mkimbizi.
Jitayarishe kabla ya kusimulia hadithi yako kwenye mahojiano yako ya kujua kama unastahiki kuwa mkimbizi. Ni muhimu kuhakikisha kwamba hadithi yako isibadilike wakati wote wa dai lako. Ukikosea kitu au kuacha jambo lolote, zungumza na mwakilishi wako wa kisheria. Weka nakala za hati zote unazopokea kutoka kwa serikali kuhusu dai lako la ukimbizi.
Eleza hadithi yako
Unaweza kulazimika kusimulia hadithi yako mara nyingi na kwa watu tofauti. Wanaweza kuwa maafisa wa CBSA , maafisa wa IRCC, mwakilishi wako wa kisheria, na Mwanachama wa IRB-RPD wakati wa kusikilizwa kwako. Hii inaweza kukufanya uhisi woga. Jitahidi kuwa mwaminifu na mkweli kuhusu hadithi yako. Jaribu kuhakikisha kuwa hadithi yako ni thabiti iwezekanavyo.
Ushauri kutoka kwa ndugu na marafiki
Ushauri wa kisheria unapaswa kutoka kwa mwakilishi wako wa kisheria. Ushauri kutoka kwa familia na marafiki, hata kama waliotoa madai ya ukimbizi, huenda usiwe sahihi kwako. Wakati mwingine, watu wanaojaribu kusaidia huwa hawana uzoefu wa kutosha. Kila dai la mkimbizi ni tofauti. Ikiwa huna mwakilishi wa kisheria, tafuta mfanyakazi wa ofisi ya kusaidia wageni unayemwamini akupe taarifa.
