Chukua Hatua: Jifunze, Jiunganishe, na Jitayarishe
Jifunze vidokezo vya jinsi ya kuufanya mchakato wa ukimbizi. Pata taarifa nzuri. Endelea kujiunga na misaada ya kijamii. Kuwa tayari kwa kila hatua.
Anzisha Dai lako la Ukimbizi
Sehemu hii itakupa muhtasari wa jinsi dai la ukimbizi linavyoanza. Itajibu maswali ya msingi. Itakuelekeza jinsi ya kuanza dai lako.
Pata maelezo ya kina kuhusu jinsi ya kuanzisha dai lako la ukimbizi katika Sehemu ya 4 – Anza Dai Lako la Ukimbizi.
Maswali ya kawaida
Unaweza kuanza dai lako la ukimbizi wakati unawasili Kanada au ukiwa tayari uko Kanada. Unaweza kuwa na maswali mengi:
- Je, nitaanzaje dai langu la ukimbizi?
- Mchakato huu utachukua muda gani?
- Nini kitatokea ikiwa dai langu litakataliwa?
- Ni lini nitaunganishwa tena na familia yangu?
- Je, nitapataje msaada?
- Je, hadithi yangu itaaminika?
Usijali! Kuna watu wengi ambao wanaweza kukusaidia kwenye huu mchakato. Rudi kwenye tovuti hii wakati wowote ili upate msaada.
Pata usaidizi wa kisheria
Mchakato wa kudai ukimbizi unaweza kuwa mrefu na mgumu. Pata usaidizi wa kisheria haraka uwezavyo.
Pindi utakapoamua kufanya dai lako, pata usaidizi wa kisheria kujaza Fomu yako ya Msingi wa Madai (BOC). Itachukua muda kufanya kazi na mwakilishi wa kisheria ili kuweka mambo yote muhimu katika BOC yako.
Mwakilishi wa kisheria anaweza kukusaidia kujaza fomu na kutayarisha hati zote. Anaweza kwenda nawe kwenye kikao cha kusikilizwa kwa dai lako na kukusaidia kueleza hadithi yako.
Jua una chaguo gani
Fanya utafiti na upate ushauri wa kisheria kabla ya kuanza dai lako. Hakikisha kuwa kutuma dai la ukimbizi ndio chaguo bora kwako. Elewa jinsi uamuzi huu unaweza kuathiri maisha yako ya baadaye.
Makinika
Makinika na uchukue muda wako kujaza Fomu yako ya BOC. Fomu ya BOC ni muhimu sana na unaweza kulazimika kuizungumzia siku ya kusikilizwa kwa dai lako. BOC lazima ijumuishe matukio yote muhimu katika maisha yako ambayo yanaonyesha kuwa wewe ni mkimbizi.
Jijali
Kufanya madai ya ukimbizi ni kazi ngumu. Chukua mambo hatua moja baada ya nyingine. Kumbuka kujijali.
Kuwa makini
Utapokea karatasi na hati nyingi wakati wa mchakato wako wa dai la ukimbizi. Kuna faili iliyogawanywa sehemu tofauti ya kuweka hati zako na kuzipanga. Jaribu kupata moja, na uanze kuitumia.
Tengeneza nakala na uweke makaratasi yako vizuri.
Weka makaratasi na nyaraka zozote za serikali, hata kama muda wake umeisha. Huenda wewe au mwakilishi wako wa kisheria mtazihitaji.
Jitayarishe kwa mahojiano yako ya kuamua kama unastahiki kuwa mkimbizi.
Jitayarishe kabla ya kusimulia hadithi yako kwenye mahojiano yako ya kujua kama unastahiki kuwa mkimbizi. Ni muhimu kuhakikisha kwamba hadithi yako isibadilike wakati wote wa dai lako. Ukikosea kitu au kuacha jambo lolote, zungumza na mwakilishi wako wa kisheria. Weka nakala za hati zote unazopokea kutoka kwa serikali kuhusu dai lako la ukimbizi.
Eleza hadithi yako
Unaweza kulazimika kusimulia hadithi yako mara nyingi na kwa watu tofauti. Wanaweza kuwa maafisa wa CBSA , maafisa wa IRCC, mwakilishi wako wa kisheria, na Mwanachama wa IRB-RPD wakati wa kusikilizwa kwako. Hii inaweza kukufanya uhisi woga. Jitahidi kuwa mwaminifu na mkweli kuhusu hadithi yako. Jaribu kuhakikisha kuwa hadithi yako ni thabiti iwezekanavyo.
Ushauri kutoka kwa ndugu na marafiki
Ushauri wa kisheria unapaswa kutoka kwa mwakilishi wako wa kisheria. Ushauri kutoka kwa familia na marafiki, hata kama waliotoa madai ya ukimbizi, huenda usiwe sahihi kwako. Wakati mwingine, watu wanaojaribu kusaidia huwa hawana uzoefu wa kutosha. Kila dai la mkimbizi ni tofauti. Ikiwa huna mwakilishi wa kisheria, tafuta mfanyakazi wa ofisi ya kusaidia wageni unayemwamini akupe taarifa.
Andaa Taarifa Zako
Sehemu hii inakupa muhtasari kuhusu kuandaa maelezo kwa ajili ya dai lako. Itakuambia kuhusu ushahidi muhimu wa kuunga mkono hadithi yako. Itakuelezea jinsi ya kudhibiti na kueleza maelezo yako muhimu.
Jifunze zaidi kuhusu ushahidi na nyaraka muhimu katika Sehemu ya 5: Jitayarishe kwa Usikilizaji Wako.
Andika hadithi yako
Inasaidia kuandika hadithi ya kile kilichokupata na kwa nini unaogopa kurudi katika nchi yako. Panga hadithi yako kwa mpangilio, kuanzia mwanzo hadi mwisho, na ujumuishe tarehe nyingi iwezekanavyo. Hii inaweza kukusaidia kutambua ushahidi muhimu kwa dai lako. Hakikisha umejumuisha kila jambo muhimu na usikose kueleza taarifa yoyote. IRB-RPD inaweza kukataa ikiwa utazuia maelezo au utawasilisha maelezo mapya kwenye usikilizaji wako.
Kusanya ushahidi wako
Ni muhimu kukusanya ushahidi wa kuunga mkono dai lako. Ushahidi husaidia IRB-RPD kuamini kilichotokea kwako, na kuelewa hali katika nchi yako na kwa nini huwezi kurudi.
Baadhi ya mifano ya ushahidi unoaweza kukusanya ni:
- Nyaraka zinazothibitisha wewe ni nani
- Ushahidi unaoonyesha kilichotokea kwako ni kweli
- Hati au ripoti za habari zinazoonyesha jinsi nchi yako ilivyo na kwa nini uko hatarini huko
- Barua au hati za kisheria (hati za kiapo) kutoka kwa watu wanaoweza kusema kuwa hadithi yako ni ya kweli
- Ripoti zinazoonyesha kuwa uliuliza usaidizi kutoka kwa wakala wa serikali katika nchi yako
Jaribu kupata chochote unachohitaji kutoka nchi yako (nchi yako au mahali ulipoishi kwa muda) haraka iwezekanavyo. Kupata ripoti za polisi au hospitali kunaweza kuchukua muda mrefu. Ikiwa huwezi kupata kitu, weka rekodi ya jinsi ulivyojaribu kukipata.
Kagua hati zako na ushahidi wako
Ni muhimu kusoma ushahidi na nyaraka zako zote ili kutafuta makosa. Mtu anaweza kukuandikia barua ya usaidizi ambayo hailingani na maelezo yaliyoko katika Fomu yako ya BOC. Huenda ukahitaji kuzungumza na mwandishi huyo ili uweze kueleza kwenye usikilizaji wako. Zungumza na mwakilishi wako wa kisheria kuhusu nini cha kufanya. Ni muhimu sana kwamba IRB-RPD waamini sehemu zote muhimu za hadithi yako.
Tafsiri hati zote
Ushahidi wote lazima utafsiriwe kwa Kiingereza au Kifaransa. Hii inachukua muda kwa hivyo ifanye haraka iwezekanavyo. Wasiliana na mwakilishi wako wa kisheria kuhusu unachohitaji kutafsiri.
Weka nakala za hati zako zote
Hifadhi nakala za hati zako zote:
- BOC yako na fomu nyingine za uhamiaji
- Hadithi yako
- Ushahidi wote, maombi yote na barua zote ambazo wewe au mwakilishi wako wa kisheria mutapeana kwa IRB, CBSA au IRCC.
Pata faili ya kuweka hati zako salama na kuzipanga. Weka hati zako hadi uwe raia wa Kanada.
Weka anwani yako sahihi
Hakikisha anwani yako ni sahihi kila wakati. Hii ni muhimu ili usikose taarifa yoyote kuhusu dai lako.
Shirikiana na Mwanasheria Wako au Mwakilishi Mwingine wa Kisheria:
Sehemu hii inakupa muhtasari kuhusu uwakilishi wa kisheria katika mchakato wa kudai ukimbizi. Inakusaidia kuelewa wajibu wako na jinsi ya kushirikiana na mwakilishi wako wa kisheria.
Jifunze maelezo ya kina kuhusu uwakilishi wa kisheria katika Sehemu ya 3 – Pata Mwakilishi wa Kisheria.
Pata mwakilishi wa kisheria
Mchakato wa kudai ukimbizi ni mgumu. Mwakilishi wa kisheria anaweza kukusaidia na kukuongoza katika mchakato huu.
Jihadhari kwa kutumia mwakilishi wa kisheria aliyeidhinishwa! Kuwa mwangalifu kuhusu watu wanaosema wanaweza kukusaidia, lakini huenda wasiwe wakili halisi au washauri wa uhamiaji.
Omba msaada kutoka kwa kliniki ya kusaidia watu kisheria ikiwa inapatikana mahali ulipo.
Kuwa mkweli
Kuwa wazi na mwaminifu kwa mwakilishi wako wa kisheria. Itakuwa vigumu kwake kukusaidia ikiwa utaficha habari. Kazi yake ni kukuongoza.
Jitayarishe
Jitayarishe kabla ya kila mkutano na mwakilishi wako wa kisheria. Unaweza kutaka kumtumia maswali kwenye barua pepe au kuandaa orodha ya maswali ya kupeleka kwenye mkutano. Hii itakusaidia kutumia muda wako vizuri.
Hili ni dai lako la ukimbizi
Kumbuka kwamba hili ni dai LAKO la ulinzi wa wakimbizi. Hata kama una mwakilishi wa kisheria, unapaswa kuhusika katika hatua zote kabla ya kusikilizwa kwako. Fuatilia tarehe za mwisho. Ukikosa tarehe moja, IRB inaweza kusema kwamba umetelekeza dai lako.
Chukua udhibiti wa kile unachoweza. Hakikisha unauelewa mchakato. Hii itafanya iwe rahisi kukubali matokeo.
Shirikiana na Mwanasheria Wako
Ni muhimu kuwa na uhusiano wa heshima na uaminifu na mwakilishi wako wa kisheria. Hivi mutaweza kufanya kazi vizuri pamoja. Zungumza na mwakilishi wako wa kisheria kuhusu mara ngapi utakutana nae na kupokea habari kuhusu kesi yako. Jua jinsi na wakati wa kuwasiliana na mwakilishi wako wa kisheria.
Jukumu la mwakilishi wako wa kisheria
Jua kile mwakilishi wako wa kisheria anaweza kufanya na nini hawezi kufanya. Usitarajie akuambie ikiwa dai lako litakubaliwa. Usitarajie akuahidi kwamba dai lako litakubaliwa. Mwanachama wa IRB-RPD ndiye ataamua kama dai lako litakubaliwa au la.
Mbadilishe Mwanasheria Wako
Una haki ya kubadilisha mwakilishi wako wa kisheria ikiwa unafikiri hakusaidii. Ikiwa huna raha, pata mwakilishi mpya. Ni muhimu kupata mtu unayeweza kumuamini.
Kipindi cha Kusubiri
Sehemu hii inakupa mawazo muhimu kuhusu jinsi ya kutumia muda wako vizuri, hasa unaposubiri kusikilizwa kwa dai lako la ukimbizi.
Kuwa na subra
Kusubiri ni sehemu ya kawaida ya kufanya madai ya ukimbizi. Huenda ukalazimika kusubiri kusikilizwa kwa dai lako au kusubiri ili kujua ikiwa dai lako litakubaliwa.
Jitayarishe
Tumia muda wa kusubiri ili kujiandaa kwa ajili ya kusikilizwa kwako:
- Hudhuria Ziara ya Kujitayarisha Kusikizwa ya IRB-RPD. Utajifunza jinsi ya kujiandaa kwa mkutano wako wa kusikilizwa na kile kitakachotokea wakati wa kusikilizwa. Pia utapata kukutana na wafanyakazi wa IRB na kuuliza maswali kuhusu kusikilizwa
- Pitia fomu yako ya BOC, simulizi yako pamoja na ushahidi uliotuma.
- Tafuta maelezo yoyote ambayo hayalingani katika fomu yako ya BOC, hadithi yako, madokezo ya mahojiano, ushahidi na hati nyingine (pamoja na maombi ya visa ya ng’ambo). Mwambie mwakilishi wako wa kisheria. Unaweza kutaka kutuma mabadiliko kwa IRB-RPD.
- Endelea kufuatilia habari kutoka kwa nchi yako. Jambo likitokea ambalo linahusiana na dai lako, mwambie mwakilishi wako wa kisheria.
Anza maisha upya
Tumia wakati huu wa kungojea kuanza maisha yako na ya familia yako. Unaweza:
- Boresha Kiingereza chako au Kifaransa
- Kupata kazi
- Endelea kufanya mazoezi
- Jitolee katika jamii
- Jiunge na kundi la wageni nchini
- Wajue majirani zako
Pata Usaidizi Unaohitaji
Sehemu hii inakupa maelezo ya hali ya juu na vidokezo vya kujitafutia usaidizi muhimu wakati wa mchakato wako wa madai ya ukimbizi.
Pata maelezo ya kina kuhusu programu na huduma za kijami zilizo karibu nawe.
Wakala wa kusaidia wageni nchini
Nenda kwa wakala wa kusaidia wagenii au kwenye huduma zingine za jamii ili upate usaidizi. Wanaweza kukusaidia kutafuta kazi, kupata nyumba, kutafuta shule za lugha, kusajili watoto wako shuleni, na kujifunza kuhusu huduma za bure kwa wanaodai ukimbizi.
Shirikisho la Mpango wa Afya wa Muda Mfupi (IFHP)
Kama mdai wa ukimbizi, unaweza kupata huduma ya afya kutoka kwa Shirikisho la Mpango wa Afya wa Muda Mfupi (IFHP) kama vile:
- huduma za hospitali,
- huduma kutoka kwa wataalamu wa afya,
- daktari wa macho na huduma ya meno ya dharura, na
- dawa ulizoandikiwa na daktari
Hii itaendelea hadi uweze kupata bima ya afya ya kawaida au hadi utakapolazimika kuondoka Kanada.
Pata msaada wa afya ya akili
Unaweza kuwa na mawazo mengi wakati wa mchakato wa kudai ukimbizi. Unaweza pia kuwa ulipitia mateso katika nchi yako, wakati wa safari yako kuja Kanada, au hapa Kanada. Kuna huduma hapa Kanada ambazo zinaweza kukusaidia. IFHP hutoa msaada kukusaidia na hili.
Pata marafiki wapya
Jaribu kukutana na wadai wakimbizi wengine au wageni hapa Kanada. Inaweza kusaidia kuongea na watu wengine ambao wanapitia hali kama yako. Pata marafiki wapya na uendelee kuwasiliana na familia yako na marafiki nyumbani kama unaweza.
Siku Yako ya Kusikilizwa
Sehemu hii inakupa maelezo ya hali ya juu na vidokezo vya kukusaidia kujiandaa kwa ajili ya kusikilizwa kwa ukimbizi wako.
Pata maelezo ya kina katika Sehemu ya 6 – Katika Usikilizaji Wako.
Jijali
Jichunge vizuri siku yako ya kusikizwa (kwa mfano, hakikisha umepata usingizi wa kutosha).
Tarajia maswali
Kuwa tayari kujibu maswali kuhusu dai lako. Kwa mfano, unaweza kuulizwa kwa nini hukutoa madai yako ya ndani ya nchi mapema kuliko ulivyofanya.
Wanachama ni watu pia
Mwanachama wa IRB-RPD ndiye anayeamua dai lako. Kila Mwanachama ni tofauti, kila dai ni tofauti, lakini kila uamuzi unapaswa kuwa wa haki.
Itisha mda wa mapumziko
Ni kawaida kuhisi woga au kuwa na hisia nyingi wakati wa kusikizwa kwako. Ikiwa unahisi hasira unaweza kuomba upewe mda wa kupumzika. Mwanachama amefunzwa kuelewa kwamba kuzungumza kuhusu hali yako kunaweza kuwa vigumu.
Jibu maswali moja kwa moja
Kuwa mwaminifu unapojibu maswali wakati wa kusikilizwa kwako. Usiwahi kutunga jibu la uongo. Ikiwa hujui kitu, au huna uhakika, sema hivyo.
Ikiwa hauelewi swali lolote, usijaribu kulijibu. Mwambie Mjumbe huelewi na umwambie akuulize tena kwa njia tofauti.
Fanya kazi na mkalimani
IRB-RPD itakupatia mkalimani mtaalamu bila malipo anayezungumza lugha yako na lahaja yako wakati wa kusikilizwa kwako. Hata kama unaelewa Kiingereza au Kifaransa, ni wazo zuri kuwa na mkalimani ili kuepusha makosa. Mkalimani anahakikisha kwamba kila mtu anaeleweka vizuri. Kabla ya mkutano wa kusikilizwa kuanza, zungumza na mkalimani wako ili uhakikishe kwamba mnaelewana vyema. Ikiwa humuelewi mkalimani, au umeona mkalimani amekosea, mwambie Mjumbe mara moja. Unapozungumza wakati wa kusikilizwa, tumia sentensi fupi fupi kwa ajili ya makalimani.
Mikutano ya mtandaoni
Mikutano mengi ya wakimbizi hufanywa mtandaoni (mkutano wa video). Utahitaji:
- Mtandao wa kuaminika, salama na wa kasi ya juu
- Kompyuta, au kifaa chenye kamera inayofanya kazi
- Sehemu ya utulivu na ya faragha
Ikiwa usikilizaji wako umeratibiwa ufanywe kutumia video lakini huna nafasi ya faragha au kompyuta unayoweza kutumia, unaweza kuuliza IRB-RPD wakupe kompyuta na chumba katika ofisi zao utumie. Unaweza pia kuuliza IRB-RPD usikilizwe ana kwa ana ikiwa unahisi hii itakuwa bora kwako.
Baada ya Kusikizwa kwako
Sehemu hii itakupa maelezo ya hali ya juu na vidokezo kuhusu kile kitachotokea baada ya kusikilizwa kwako.
Kama utapata uamuzi mzuri au hasi, unaweza kupata maelezo ya kina ya hatua zinazofuata katika Sehemu ya 7 – Baada ya Kusikizwa Kwako.
Uamuzi
Mwanachama anaweza kufanya maamuzi kuhusu dai lako mwishoni mwa kusikilizwa kwako. Au anaweza kusema kwamba atakutumia uamuzi wako kwenye barua. Hii inaweza kukupa presha, lakini haimaanishi kuwa una uwezekano mkubwa wa kukataliwa.
IRB-RPD itatuma Notisi ya Uamuzi iliyoandikwa pamoja na sababu za uamuzi huo.
Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, Notisi ya Uamuzi itatumwa kwake kupitia My Case. Atakushirikisha.
Ikiwa unajiwakilisha mwenyewe, IRB-RPD itatuma Notisi ya Uamuzi moja kwa moja kwako kupitia My Case. Ikiwa bado huna My Case, watakutumia uamuzi huo kwa posta.
Ukikataliwa
Kuna mambo ya kisheria ya kufanya ikiwa dai lako limekataliwa. Zungumza na mwakilishi wako wa kisheria.
Tuma ombi la kuwa mkazi wa kudumu
Dai lako la ukimbizi likikubaliwa, tuma ombi la ukaaji wa kudumu mara moja. Fanya hivi kwa ajili yako na familia yako. Ukichelewa, unaweza kupata matatizo kama vile kuomba upewe kibali cha kazi kingine. Kumbuka, ukipata ulinzi wa wakimbizi, huwezi kurudi katika nchi yako. Ukifanya hivi, serikali inaweza kutuma dai lako kwa IRB-RPD ili usikilizwe tena.