Vikao vya kusikiliza madai ya ukimbizi huwa viko aina mbili: vikao vya mtandaoni, na vikao vya ana kwa ana.
Vikao vya Mtandaoni
Vikao vya mtandaoni huwa vinafanywa kwenye mtandao. Mikutano hii hufanyika kwenye kompyuta kutumia Microsoft Teams.
Jitayarishe kwa ajili ya kikao chako cha mtandaoni
Baada ya IRB-RPD kuamua kikao chako kitafanywa siku gani na ni saa ngapi, watakutumia barua ya kukupa taarifa au watamtumia mwakilishi wako wa kisheria. Soma taarifa hii kwa uangalifu kwa sababu itakuelezea ni nini cha kufanya ili uwe uko tayari kuhudhuria kikao chako cha mtandaoni.
Ili kufanya mkutano wako mtandaoni utahitaji:
- Mtandao wa kuaminika, ulio salama, na wa kasi ya juu
- Tarakilishi au kompyuta
- Sehemu ya utulivu na ya siri
Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, unaweza kwenda ofisini kwake kuufanya mkutano huu. Jadiliana na mwakilishi wako wa kisheria ili ujue kama hii itawezekana.
Iwapo hutaenda kwa afisi ya mwakilishi wako wa kisheria, hakikisha kuwa una kila kitu unachohitaji ili kuufanya mkutano wako mtandaoni. Ikiwa huna tarakilishi au kompyuta, au huna mtandao, omba usaidizi kutoka kwa IRB-RPD. IRB-RPD wanaweza kukupa tarakilishi na chumba katika ofisi zao ili utumie. Tuma maombi kwa ofisi ya IRB-RPD iliyo katika eneo lako kwa kupiga simu, au kutuma barua, au barua pepe. Lazima uwasiliane nao kwa muda usiopungua wiki mbili kabla ya tarehe ya mkutano wako kufika.
Takriban siku tano kabla ya mkutano wa kusikiliza dai lako, IRB-RPD watamtumia mwakilishi wako wa kisheria tovuti ya kujiunga kwenye mkutano wa kikao chako cha mtandaoni. Mwakilishi wako wa kisheria atakupa tovuti hii. Ikiwa huna mwakilishi wa kisheria, IRB-RPD watakutumia tovuti hiyo kwenye barua ya pepe. Hakikisha kuwa IRB-RPD wana maelezo sahihi ya anwani ya kukutumia barua na barua pepe, pamoja na nambari ya simu unayoitumia.
Katika kikao chako cha mtandaoni
Siku ya kikao cha mtandaoni cha kusikiliza dai lako, utaombwa ujiunge kwenye mkutano dakika 15 kabla ya mkutano huo kuanza. Hii itakupa nafasi ya kuhakikisha kwamba mtandao wako wa intaneti unafanya kazi vyema, utakuwa na muda wa kusalimiana na mfanyakazi wa IRB-RPD, na pia utapata fursa ya kuongea na mkalimani wa IRB ili uhakikishe kuwa mnaelewana kilugha. Mwanachama wa IRB atakapojiunga kwenye mkutano, atazungumza na wewe na kukuuliza uthibitishe kuwa uko peke yako na uko mahali pa faragha. Ikiwa una matatizo yoyote ya kuona au kusikia video wakati wa kikao hiki cha mtandaoni, hakikisha umemjulisha Mwanachama.
Ikiwa hutaki mkutano wako ufanyike mtandaoni
Mikutano ya kusikiliza maombi ya wakimbizi yote huwa yamepangwa yafanyike mtandaoni, lakini kikao chako kinaweza kubadilishwa kikafanywa ana kwa ana.
Lazima ujaze fomu hii na uitume angalau siku kumi kabla ya siku ya kusikilizwa kwa ombi lako. Lazima useme ni kwa nini unataka mkutano wako ufanywe ana kwa ana.
Mikutano ya ana kwa ana
Mikutano ya ana kwa ana huwa inafanyika katika ofisi ya IRB-RPD. Wakati wa mkutano, kila mtu atakuwa yuko kwenye chumba kimoja.
Mkutano wako utafanywa ana kwa ana ikiwa IRB-RPD wataamua hivyo au ikiwa ulituma ombi kikao chako kifanywe ana kwa ana na IRB-RPD wakakubali.
Mikutano ya ana kwa ana hufanyika katika ofisi za IRB-RPD. Baada ya IRB-RPD kuchagua tarehe na saa ya mkutano wako, watakutumia wewe au mwakilishi wako wa kisheria Taarifa ya Kuhudhuria mkutano. Taarifa ya Kuhudhuria mkutano itakupa anwani ambapo mkutano huo utafanyika. Soma taarifa hii kwa uangalifu kwa sababu itakuelezea ni nini cha kufanya.
Katika mkutano wako wa ana kwa ana
Siku ya mkutano wako wa ana kwa ana, hakikisha umewasili angalau dakika 15-30 kabla ya mkutano wako kuanza. Hii itakupa muda wa kukitambua chumba ambacho mkutano utafanyika. Ikiwa una watu waliokuja kukuangalia au una mashahidi wowote, wao pia wanapaswa wafike angalau dakika 15 kabla ya mkutano kuanza. Unaweza kuulizwa usubiri katika chumba cha wageni hadi chumba cha mkutano kiwe tayari. Kabla ya mkutano wako kuanza, fanya mazungumzo na mkalimani ili uhakikishe kuwa mnaelewana lugha.
