Mwanachama wa IRB-RPD ataangalia ukweli katika kesi yako na hali katika nchi yako ilivyo ili kuamua kama unahitaji ulinzi. Kuna masuala muhimu ya kisheria ambayo Mwanachama anaweza kuzungumzia kwenye kikao chako cha mkimbizi. Soma masuala haya ya kisheria katika sehemu iliyo hapa chini.
Lazima uonyeshe kuwa wewe ni yule mtu unayesema. Hii inamaanisha ni lazima uonyeshe hati zinazothibitisha kuwa wewe ni raia wa nchi yako. Lazima pia uonyeshe hati kuhusu hali yako ya uhamiaji ikiwa umeishi katika nchi nyingine.
Inaweza pia kuwa muhimu kuonyesha dini yako au asili ya kabila, uanachama wako wa kitaaluma, kisiasa, au muungano, mwelekeo wa ngono, au uanachama wako katika aina nyingine ya kikundi cha kijamii.
Ikiwa huwezi kupata baadhi ya hati za kuthibitisha wewe ni nani, itabidi ueleze ni kwa nini kwenye kikao chako. Unaweza kueleza jinsi ulivyojaribu kupata ushahidi.
Mfano wa ushahidi
Hapa kuna mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kuonyesha utambulisho wako:
- Ili kuthibitisha kuwa wewe ni raia wa nchi yako:
- Pasipoti
- Kitambulisho cha taifa
- Kadi ya huduma ya kijeshi
- Cheti cha ndoa
- Nakala za shule
- Mashahidi kutoka nchi yako wanaokujua wewe au familia yako
- Ili kuthibitisha dini yako:
- Cheti cha ubatizo
- Barua kutoka kwa kiongozi wako wa kidini
- Ili kuthibitisha kikundi chako cha kisiasa au kitaaluma:
- Kadi ya uanachama katika chama cha siasa au kikundi kingine
- Barua kutoka kwa shirika
- Nakala zinazoonyesha mafunzo ya kitaaluma
- Rekodi za biashara
- Diploma
- Ili kudhibitisha mwelekeo wako wa kijinsia:
- Barua kutoka kwa kikundi cha jumuiya, mshirika, au mwanafamilia.
- Mashahidi ambao wanaweza kutoa maelezo kuhusu jinsi wanavyojua wewe ni mtu wa jumuiya ya LGBTQ.
Lazima uonyeshe kwamba unasema ukweli na kwamba ushahidi wako wote ni wa kweli.
Ili kuamua kama wanaweza kukuamini, mwanachama wa IRB-RPD anahitaji kuona kwamba maelezo yote katika dai lako yanalingana. Mwanachama atalinganisha:
- Fomu yako ya BOC na hadithi yako,
- ushahidi wako
- utakachosema kwenye masikizo yako,
- mashahidi wako watasema nini, na
- habari na ripoti za haki za binadamu.
Ikiwa kuna tofauti ambazo huwezi kuzielezea, Mwanachama anaweza kuamua kwamba hawezi kuaminika. Hii inaweza kudhuru majaribio mengine yoyote unatakayofanya ya kubaki Kanada.
Mifano ya ushahidi
Hapa kuna mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kuonyesha unasema ukweli na kuaminika:
- Ripoti za nchi na nakala za habari kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu
- Rekodi za matibabu/hospitali au risiti
- Ripoti za polisi
- Picha za majeraha
- Taarifa za mashahidi
- Barua kutoka kwa daktari wako nchini Kanada kuhusu makovu au majeraha
- Picha za kutoka kwa mitandao ya kijamii
- Picha za meseji za simu zinazoonyesha vitisho dhidi yako
Vidokezo vya kukusaidia kuonyesha kuwa unasema ukweli kwenye kikao chako:
- Kuwa na ushahidi unaoonyesha maelezo fulani ya hadithi yako ni ya kweli.
- Kuwa mwangalifu usiongeze chumvi au kupamba hadithi yako.
- Usijibu swali lolote ambalo huelewi.
- Ikiwa huelewi swali muulize Mwanachama alirudie au atumie maneno tafauti
- Kuwa mwaminifu. Usibahatishe.
- Jibu kwa sentensi ndefu na kamili ili kuhakikisha kuwa Mwanachama anakuelewa.
- Chagua mashahidi wako kwa uangalifu. Waambie lazima waseme ukweli. Waeleze kuwa Mwanachama atatarajia wanachosema kilingane na unachosema wewe. Unaweza kuwapa mashahidi wako nakala ya ushahidi wako.
Lazima uonyeshe kwamba kweli unaogopa kutendewa vibaya ikiwa utarudi katika nchi yako. Hii pia inajulikana kama “hofu ya kibinafsi.” Hapa kuna baadhi ya mifano ya maswali ambayo Mwanachama anaweza kukuuliza:
- Baada ya kutendewa vibaya katika nchi yako, kwa nini hukuondoka mara moja?
- Kwa nini ulipitia nchi nyingine salama ulipokuwa unaelekea Kanada (kwa mfano, Marekani), lakini hukutoa dai?
- Kwa nini ulirudi katika nchini yako baada ya kuondoka?
- Kwa nini ulisubiri kutoa dai baada ya kufika Kanada?
Fikiria juu ya maswali haya na majibu yako. Jitayarishe kadri uwezavyo kabla ya kusikilizwa kwako. Je, una ushahidi ambao utakusaidia kueleza ulichofanya au kutofanya? Kwa mfano, ulitumaini kwamba hali katika nchi yako ingebadilika? Je, ilikuwa vigumu kuondoka katika nchi yako?
Mifano ya ushahidi
Hapa kuna baadhi ya mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kusaidia kuonyesha kwa nini unaogopa kurudi katika nchi yako:
- Ripoti za polisi zinazoonyesha ulitafuta usaidizi kwa polisi au uliripoti uhalifu dhidi yako
- Ripoti za daktari za matibabu yoyote au majeraha
- Uthibitisho kwamba ulijaribu kutoroka hatari (kama vile tikiti, risiti, hati za kusafiri)
- Taarifa za mashahidi kwamba ulijaribu kujikinga na vitisho
- Taarifa ulizokusanya kuhusu kutoa dai katika nchi nyingine
- Hati zinazoonyesha kwa nini hukuweza kuondoka nchi yako mapema
- Hati zinazoonyesha kuwa ulipata tabu kutuma madai nchini Kanada mara tu ulipowasili
- Uthibitisho wako wa kuwasili na kuingia Kanada
Ni lazima uonyeshe kwamba wewe binafsi unakabiliwa na hatari ya kuteswa au kudhuriwa katika nchi yako. Lazima uonyeshe kuwa hii sio hatari ya jumla katika nchi yako. Kwa mfano, ikiwa kuna vurugu nyingi, lazima uonyeshe kwa nini wewe binafsi uko hatarini. Ukiweza, taja ni nani (au kikundi gani) kimekulenga, kwa nini, na unajuaje.
Lazima pia uonyeshe kuwa uko hatarini kwa sababu ya rangi yako, dini, utaifa, maoni ya kisiasa, au uanachama wako katika kikundi cha kijamii. Hii inaitwa misingi ya Mkataba. Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, muulize ni sababu zipi zinaweza kutumika kwako.
Mifano ya ushahidi
Hii hapa ni baadhi ya mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kuonyesha kuwa uko katika hatari ya kudhuriwa katika nchi yako:
- Vidokezo vyovyote, barua, ujumbe wa simu unaoonyesha vitisho vya vurugu
- Taarifa rasmi kutoka kwa mashahidi wakisema kwamba wewe, au watu kama wewe, mmekuwa waathirika wa ukatili
- Picha za majeraha au aina nyingine za uharibifu
- Picha za uporaji au uharibifu ulioona (au ulioshiriki)
- Rekodi za matibabu
- Ripoti za polisi kutoka kwa nchi yako
- Ushahidi wa mitandao ya kijamii au video (ikiwa video ina mtu yeyote anayezungumza, maneno hayo lazima yaandikwe na kutafsiriwa kwa Kiingereza au Kifaransa)
Lazima uonyeshe kuwa serikali yako haiwezi au haitaki kulinda.
Ikiwa ulijaribu kupata ulinzi kutoka kwa watu wenye mamlaka katika nchi yako lakini haukuupata:
- Eleza ni nini ulichofanya na jinsi walivyokujibu.
- Jaribu kupata hati zinazoonyesha kwamba ulijaribu kupata usaidizi.
- Jaribu kutafuta ripoti kutoka nchi yako zinazoonyesha kwamba mamlaka yenu haiwezi au haitaki kulinda watu kama wewe.
Iwapo hukujaribu kupata ulinzi kutoka kwa mamlaka ya nchi yako:
- Eleza kwa nini na ujaribu kupata hati zinazo onyesha kwamba haikuwa busara kufanya hivyo.
- Toa mifano ya kile kilichotokea kwa watu wengine ambao walijaribu kuomba msaada.
Mifano ya ushahidi
Hapa kuna baadhi ya mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kuonyesha kwa nini serikali yako haiwezi kukulinda:
- Ripoti za nchi au habari zinazoonyesha ufisadi wa serikali au ukosefu wa ulinzi kutoka kwa polisi
- Ripoti ulizotoa kwa polisi
- Kauli kutoka kwa watu walio katika hali kama yako. (Ni vyema wakisema kuwa ni ukweli mbele ya mwanasheria au mthibitishaji wa umma. Pia waombe nakala ya kitambulisho chao.)
Lazima uonyeshe kwamba si salama au haiwezekani kwako kuishi katika sehemu yoyote ya nchi yako.
IRB-RPD inaweza kutaja jiji katika nchi yako ambapo wanafikiri unaweza kuhamia na kuishi kwa usalama. Hii inajulikana kama “sehemu mbadala ya ndani ya nchi ya kuhamia” Lazima uonyeshe kwamba:
- huwezi kuishi huko kwa usalama, au
- haitakuwa jambo la busara kwako kuishi huko (kwa sababu ya umri wako, jinsia, au hali, kwa mfano).
Mifano ya ushahidi
haitakuwa jambo la busara kwako kuishi huko (kwa sababu ya umri wako, jinsia, au hali, kwa mfano).
- Hati zinazoonyesha ulijaribu kujiepusha na matatizo kwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yako.
- Ripoti zinazoonyesha tatizo hilo liko nchi nzima. Kwa mfano, watu unaowaogopa wako kote nchini, au matendo unayoogopa yapo katika sehemu zote za nchi yako.
- Ripoti zinazoonyesha kwa nini mtu kama wewe angeona vigumu kuishi katika eneo hilo. Kwa mfano, ripoti zinazoelezea utamaduni katika nchi yako au kuonyesha kwamba kuna matatizo makubwa katika eneo hilo.
- Barua kutoka kwa marafiki au jamaa waliokusaidia kujificha katika sehemu mbalimbali za nchi yako.
- Ripoti zinazoonyesha kwamba hakuna njia ya kufika katika eneo hilo, kwa sababu ya vita, maafa ya asili, au sababu nyinginezo.
Ni lazima uonyeshe kuwa uko hatarini katika kila nchi ambayo wewe ni raia au mkazi wa kudumu.
Iwapo IRB-RPD itagundua kuwa uko hatarini katika nchi moja, lakini unaweza kuishi kwa usalama katika nchi nyingine ambako wewe ni raia au mkazi wa kudumu, watakataa dai lako. Pia watakataa dai lako ikiwa una hadhi ya mkimbizi katika nchi iliyotia saini Mkataba wa Wakimbizi na unaweza kurudi huko.
Mifano ya ushahidi
Hapa kuna baadhi ya mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ikiwa IRB-RPD inafikiri unaweza kuishi kwa usalama katika nchi nyingine:
- Ikiwa una haki ya kuishi katika nchi zaidi ya moja, fikiria aina ya hatari utakayokabiliana nayo katika kila nchi. Tuma ushahidi mwingi uwezavyo kuhusu hatari hiyo.
- IRB-RPD inaweza kufikiria kuwa una haki ya kuishi katika nchi nyingine. Ikiwa unafikiri wewe si raia tena au mkazi wa kudumu wa nchi hiyo, ipe IRB-RPD hati ya serikali inayoonyesha hili
- Iwapo hukuwahi kuwa raia nchi ambayo ulizaliwa, wape IRB-RPD nakala ya sheria ya uraia wa nchi hiyo. (Unaweza kupaita sheria hii kwenye mtandao.)
- Iwapo ulipoteza hadhi yako ya ukaaji wa kudumu au hadhi yako ya ukimbizi katika nchi, ipe IRB-RPD hati ya serikali inayoonyesha kuwa huwezi kurudi huko.
IRB-RPD inaweza kukataa dai lako kwa sababu ya uhalifu. Hii inaitwa kutengwa. Hii inaweza kutokea ikiwa IRB-RPD inafikiri ume:
- ulifanya uhalifu wa kivita,
- ulifanya uhalifu mkubwa usio wa kisiasa nje ya Kanada, au
- ulivunja sheria za kimataifa za haki za binadamu.
Hakikisha unazungumza na wakili ikiwa IRB-RPD itakuambia kuwa watakuwa wanachunguza uhalifu kama sehemu ya dai lako la ukimbizi.
Mifano ya ushahidi
Hapa kuna baadhi ya mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ikiwa IRB-RPD itasema umehusika katika shughuli za uhalifu:
- Rekodi ya mahakama ya hatia yoyote
- Rekodi za polisi za ukweli ambao uliripotiwa kwao kwanza
- Taarifa za mashahidi kuhusu mashtaka
- Maoni ya kisheria kutoka kwa mwanasheria kutoka nchi yako
Ikiwa hukutoa dai la ukimbizi mara tu ulipowasili Kanada, lazima ueleze ni kwa nini ulichelewa kufanya hivyo. Unaweza kuulizwa ueleze kwa nini hukuondoka nchini kwako mapema, kutoa madai katika nchi nyingine, au kutoa dai la ukimbizi mara tu ulipowasili Kanada.
Ni muhimu kufikiria jinsi utakavyoweza kujibu maswali haya kwa sababu IRB-RPD inaweza isiamini kuwa kwa kweli unaogopa kurudi katika nchi yako ikiwa ulichelewa kutoa dai lako.
Ikiwa hukutoa dai la ukimbizi haraka, fikiria maswali yafuatayo ili ikusaidie kueleza sababu yako ya kuchelewa:.
- Je, uliogopa kurudi katika nchi yako muda fulani baada ya kufika Kanada?
- Je, hukujua kwamba unapaswa kutoa dai mara tu unapowasili Kanada?
- Je, ulipata tabu kutoa dai au kupata mwakilishi wa kisheria?
- Je, hukujua jinsi ya kutoa madai na ilikuchukua muda kujua?
Toa maelezo na ujitahidi kueleza hali hiyo au mazingira yalivyokuwa. Kuwa tayari kujibu maswali ambayo Mwanachama anaweza kuwa nayo kuhusu kuchelewa kwako wakati wa kusikilizwa kwako.
