Jitayarishe kwa Kusikilizwa kwa Dai Lako

Jifunze ni ushahidi gani unaweza kukusanya na kuwasilisha kabla ya kusikilizwa kwa kesi yako ya wakimbizi. Elewa kile ambacho Kamati ya Uhamiaji na Wakimbizi ya Kanada (IRB) inahitaji ili kufanya uamuzi na jinsi ushahidi wako unaweza kuunga mkono dai lako la ukimbizi.

Elewa Ufafanuzi wa Kisheria

Ili dai lako la ukimbizi likubaliwe, ni lazima uonyeshe kuwa wewe ni Mkimbizi kulingana na Mkataba wa Geneva au Mtu Anayehitaji Ulinzi. Mwanachama wa IRB-RPD atafanya uamuzi baada ya kusoma hati zako na kusikiliza hadithi yako.

Unahitaji kuelewa ufafanuzi na jinsi ya kukusanya ushahidi ili kusaidia dai lako.

Soma kila sehemu ya ufafanuzi. Kwa kila sehemu ambayo ni kweli kwako, tengeneza orodha ya ushahidi unaoweza kupata ili kuonyesha kuwa ni kweli. Mpe mwakilishi wako wa kisheria orodha hiyo.

Mkimbizi kulingana na Mkataba wa Geneva

Ili kuwa mkimbizi wa Mkataba wa Geneva, sentensi hizi sita lazima ziwe kweli kwako:

  • Nikirudi katika nchi yangu, kuna uwezekano nitakumbana na mateso (kutendewa vibaya sana).
  • Ningeteswa kwa sababu ya rangi yangu, dini, utaifa, maoni ya kisiasa, au kwa sababu ya kikundi cha kijamii ninachotoka.
  • Kwa kweli naogopa kurudi.
  • Nina sababu nzuri ya kuogopa kuishi katika nchi yangu.
  • Serikali yangu haiwezi kunilinda.
  • Siwezi kuishi kwa usalama au kwa njia inayofaa katika sehemu nyingine yoyote nchini kwetu.

Mtu Anayehitaji Ulinzi

Ili kuwa mtu anayehitaji ulinzi, lazima uonyeshe kuwa 1 au 2 ni kweli:

  1. Nikirudi katika nchi yangu, huenda watu walio na mamlaka watanitesa. AU
  2. Nikirudi katika nchi yangu, naweza kufa au kupata mateso ya kikatili au kuadhibiwa, na…
    • Serikali yangu haiwezi kunilinda,
    • Siwezi kuishi kwa usalama au kwa njia inayofaa katika sehemu nyingine yoyote nchini kwetu.
    • Niko hatarini lakini sio kila mtu katika nchi yangu ana hatari hii,
    • Siko hatarini kwa sababu tu nchi yangu inataka kuniadhibu kwa kufanya jambo ambalo ni la uhalifu nchini Kanada, na
    • Siko hatarini kwa sababu tu ya huduma duni za afya katika nchi yangu.

Kusanya Ushahidi

Ni muhimu kukusanya na kutuma ushahidi kuhusu dai lako la ukimbizi kwa IRB-RPD. Ushahidi unajumuisha habari yoyote inayoonyesha unasema ukweli kuhusu wewe ni nani, kile ambacho tayari kimekupata, na kile ambacho unahofu kingekupata iwapo ukirudi katika nchi yako. Inaweza kuwa nyaraka, barua, makala ya magazeti, ripoti za matibabu ya kimwili au kisaikolojia, picha, rekodi za sauti, au hata video.

Ushahidi humsaidia Mwanachama kuamini kilichokupata, na kuelewa hali ilivyo katika nchi yako na kwa nini huwezi kurudi.

Wakati wa kuanza kukusanya ushahidi

Kupata ushahidi huchukua muda, hasa ikiwa unajaribu kuupata kutoka nchi nyingine. Anza kukusanya ushahidi haraka iwezekanavyo. Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, muulize ni ushahidi gani unaweza kukusaidia, muoneshe ushahidi ulionao, na umwambie auangalie. Chukua hatua haraka.

Masharti ya kutafsiri

Ushahidi wote, pamoja na rekodi za sauti, lazima ziwe kwa Kiingereza au Kifaransa. Usitumie Google kutafsiri na usitafsiri hati mwenyewe. Mfasiri mtaalamu ni bora zaidi. Ikiwa unapata huduma za kliniki ya kutoa msaada wa kisheria, gharama ya tafsiri inaweza kugharamiwa kwa sehemu au kikamilifu na kliniki hiyo. Ikiwa huna uwezo wa kulipia tafsiri, unaweza kutafuta mtu unayemwamini ambaye anajua lugha yako vizuri akutafsirie hati zako kwa Kiingereza au Kifaransa.

Mtafsiri wako lazima atie sahihi tamko ambalo unapaswa kutuma kwa IRB-RPD pamoja na hati ambayo ameitafsiri. Tamko hilo lazima liwe na:

  • jina la mtafsiri,
  • lugha na lahaja (ikiwa ipo),
  • taarifa kwamba tafsiri hiyo ni sahihi, na,
  • saini ya mfasiri.

Ushahidi wa kuunga mkono ombi lako

Kuna aina nne za ushahidi ambao unaweza kukusanya ili kuunga mkono dai lako.

Ushahidi wa kuonesha wewe ni nani

Unahitaji ushahidi wa kitambulisho chako na uraia wako. Hii inaweza kuwa:

  • pasipoti,
  • kitambulisho cha taifa,
  • cheti cha kuzaliwa,
  • cheti cha ndoa
  • hati za shule au cheti cha shule,
  • leseni ya kuendesha gari,
  • kitambulisho cha wanajeshi, au
  • uanachama wa kitaaluma au wa kidini.

Ushahidi wa aina nyingine pia unaweza kusaidia. Muulize mwakilishi wako wa kisheria ni ushahidi gani unaweza kuhitaji ili kudhibitisha wewe ni nani.

Ushahidi kuhusu madai yako

Unahitaji ushahidi ambao utaonyesha kwamba:

  • Hadithi yako na matukio yaliyoko kwenye simulizi yako ni ya kweli
  • Kwa kweli unaogopa kurudi katika nchi yako
  • Uko hatarini katika nchi yako
  • Serikali yako haiwezi kukulinda
  • Si jambo la busara au salama kwako kuishi katika jiji tofauti ndani ya nchi yako

Hapa kuna baadhi ya maswali ya kukusaidia kupata ushahidi wa kusaidia dai lako:

  • Je, una picha, barua, video, barua pepe, maandishi, au hati nyingine zinazoonyesha matatizo uliyokuwa nayo?
  • Je, ulienda polisi au kwa wakala wa serikali kupata usaidizi? Pata nakala ya ripoti ya polisi au uthibitisho wa ziara yako.
  • Je, ulipata msaada wa matibabu? Pata nakala ya rekodi za hospitali au za daktari.
  • Je, kuna nakala za habari au machapisho mtandaoni kuhusu watu au matukio yanayohusiana na dai lako?
  • Je, kuna watu walioshuhudia kilichotokea kwako? Waambie waandike taarifa inayosimulia kilichotokea na wakutumie. Ikiwezekana, waambie wathibitishe kuwa walichosema ni kweli mbele ya mwanasheria au mthibitishaji wa umma. Pia, waombe nakala ya kitambulisho chao.
  • Je, kuna watu ambao wamepitia matatizo kama yako? Waambie waandike taarifa inayosimulia kilichotokea na wakutumie. Ikiwezekana, waambie wathibitishe kuwa walichosema ni kweli mbele ya mwanasheria au mthibitishaji wa umma.
  • Je, madai yako yanatokana na kundi lako la kidini au la kisiasa, au kundi lingine ambalo wewe ni mwanachama? Pata hati zinazoonyesha uanachama wako.
  • Je, una matatizo ya ki akili kwa sababu ya kile kilichotokea? Pata ripoti kutoka kwa daktari, mwanasaikolojia, au mshauri wa afya ya akili nchini Kanada. Hii inachukua muda, kwa hivyo fanya hivi haraka uwezavyo.
  • Je, uko kwenye mitandao ya kijamii? Piga picha za machapisho yoyote kwenye mtandao yanayohusiana na hadithi yako.

Huenda usiweze kupata ushahidi wote unaotaka kutoka nchi yako kwa sababu si salama kufanya hivyo, au kwa sababu ni vigumu sana kuupata. Jaribu uwezavyo ili upate ushahidi, na kama huwezi kupata ushahidi fulani, eleza kwa maandishi kwa IRB kwa nini hukuweza kuupata.

Ushahidi kuhusu hali ya nchi ilivyo

Unaweza kuwasilisha ushahidi unaoonyesha hali katika nchi yako ilivyo na jinsi yanavyohusiana na dai lako. Hii inajumuisha ripoti za kuaminika kuhusu hali ya kisiasa, kijamii, kitamaduni, kiuchumi na haki za binadamu katika nchi yako.

IRB-RPD huhifadhi hati za umma kuhusu hali ilivyo katika nchi zote ulimwenguni katika Vifurushi vya Nyaraka vya Kitaifa (NDPs).

Jihadhari! Baadhi ya hati katika NDP zinaweza kuwa ni za zamani. Huenda hali katika nchi yako imebadilika au uliyoyapitia huenda yasiwe katika NDP. Zungumza na mwakilishi wako wa kisheria ili kuona ni maelezo gani mapya yanaweza kusaidia dai lako.

Kwa mfano, unaweza kutuma:

  • makala ya habari au video za hivi karibuni,
  • taarifa kutoka kwa mashahidi wa kitaalamu,
  • makala za kitaaluma, au
  • ripoti za haki za binadamu.

Tazama Vifurushi vya Nyaraka vya Kitaifa za nchi yako.

Ushahidi kutoka kwa mashahidi

Unaweza kuwa na mashahidi katika kusikilizwa kwako watakaozungumza kuhusu madai yako. Shahidi ni mtu ambaye ana taarifa muhimu kuhusu wewe na dai lako. Wakati wa kusikilizwa kwako, mashahidi watajibu maswali kutoka kwa wakili wako na kutoka kwa Mwanachama. Mashahidi hawawezi kusikiliza unachosema wewe kwenye kesi na huwezi kuzungumza nao wakati wa mapumziko. Wakati mwingine Mwanachama anaweza asihitaji kuwauliza mashahidi wako wazungumze.

Ikiwa una shahidi, toa taarifa ifuatayo kwa maandishi kwa IRB-RPD, angalau siku kumi kabla ya tarehe yako ya kusikilizwa.

  • Maelezo yao ya mawasiliano (anwani, nambari ya simu, na nambari ya faksi)
  • Taarifa fupi ikieleza kwa nini wanahitaji kuzungumza
  • Unadhani wataongea kwa mda gani
  • Uhusiano wako nao
  • Ikiwa watazungumza ana kwa ana, kupitia mkutano wa video wa mtandaoni, au kwa kutumia simu
  • Ikiwa wanahitaji mkalimani, na lugha na lahaja wanayoongea
  • Ikiwa shahidi ni mtaalam, habari kuhusu utaalamu wao, na ripoti fupi ya kile watakachosema, iliyosainiwa nao.

Ombi Lako na Masuala ya Kisheria

Mwanachama wa IRB-RPD ataangalia ukweli katika kesi yako na hali katika nchi yako ilivyo ili kuamua kama unahitaji ulinzi. Kuna masuala muhimu ya kisheria ambayo Mwanachama anaweza kuzungumzia kwenye kikao chako cha mkimbizi. Soma masuala haya ya kisheria katika sehemu iliyo hapa chini.

Lazima uonyeshe kuwa wewe ni yule mtu unayesema. Hii inamaanisha ni lazima uonyeshe hati zinazothibitisha kuwa wewe ni raia wa nchi yako. Lazima pia uonyeshe hati kuhusu hali yako ya uhamiaji ikiwa umeishi katika nchi nyingine.

Inaweza pia kuwa muhimu kuonyesha dini yako au asili ya kabila, uanachama wako wa kitaaluma, kisiasa, au muungano, mwelekeo wa ngono, au uanachama wako katika aina nyingine ya kikundi cha kijamii.

Ikiwa huwezi kupata baadhi ya hati za kuthibitisha wewe ni nani, itabidi ueleze ni kwa nini kwenye kikao chako. Unaweza kueleza jinsi ulivyojaribu kupata ushahidi.

Mfano wa ushahidi

Hapa kuna mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kuonyesha utambulisho wako:

  • Ili kuthibitisha kuwa wewe ni raia wa nchi yako:
    • Pasipoti
    • Kitambulisho cha taifa
    • Kadi ya huduma ya kijeshi
    • Cheti cha ndoa
    • Nakala za shule
    • Mashahidi kutoka nchi yako wanaokujua wewe au familia yako
  • Ili kuthibitisha dini yako:
    • Cheti cha ubatizo
    • Barua kutoka kwa kiongozi wako wa kidini
  • Ili kuthibitisha kikundi chako cha kisiasa au kitaaluma:
    • Kadi ya uanachama katika chama cha siasa au kikundi kingine
    • Barua kutoka kwa shirika
    • Nakala zinazoonyesha mafunzo ya kitaaluma
    • Rekodi za biashara
    • Diploma
  • Ili kudhibitisha mwelekeo wako wa kijinsia:
    • Barua kutoka kwa kikundi cha jumuiya, mshirika, au mwanafamilia.
    • Mashahidi ambao wanaweza kutoa maelezo kuhusu jinsi wanavyojua wewe ni mtu wa jumuiya ya LGBTQ.

Lazima uonyeshe kwamba unasema ukweli na kwamba ushahidi wako wote ni wa kweli.

Ili kuamua kama wanaweza kukuamini, mwanachama wa IRB-RPD anahitaji kuona kwamba maelezo yote katika dai lako yanalingana. Mwanachama atalinganisha:

  • Fomu yako ya BOC na hadithi yako,
  • ushahidi wako
  • utakachosema kwenye masikizo yako,
  • mashahidi wako watasema nini, na
  • habari na ripoti za haki za binadamu.

Ikiwa kuna tofauti ambazo huwezi kuzielezea, Mwanachama anaweza kuamua kwamba hawezi kuaminika. Hii inaweza kudhuru majaribio mengine yoyote unatakayofanya ya kubaki Kanada.

Mifano ya ushahidi

Hapa kuna mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kuonyesha unasema ukweli na kuaminika:

  • Ripoti za nchi na nakala za habari kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu
  • Rekodi za matibabu/hospitali au risiti
  • Ripoti za polisi
  • Picha za majeraha
  • Taarifa za mashahidi
  • Barua kutoka kwa daktari wako nchini Kanada kuhusu makovu au majeraha
  • Picha za kutoka kwa mitandao ya kijamii
  • Picha za meseji za simu zinazoonyesha vitisho dhidi yako

Vidokezo vya kukusaidia kuonyesha kuwa unasema ukweli kwenye kikao chako:

  • Kuwa na ushahidi unaoonyesha maelezo fulani ya hadithi yako ni ya kweli.
  • Kuwa mwangalifu usiongeze chumvi au kupamba hadithi yako.
  • Usijibu swali lolote ambalo huelewi.
  • Ikiwa huelewi swali muulize Mwanachama alirudie au atumie maneno tafauti
  • Kuwa mwaminifu. Usibahatishe.
  • Jibu kwa sentensi ndefu na kamili ili kuhakikisha kuwa Mwanachama anakuelewa.
  • Chagua mashahidi wako kwa uangalifu. Waambie lazima waseme ukweli. Waeleze kuwa Mwanachama atatarajia wanachosema kilingane na unachosema wewe. Unaweza kuwapa mashahidi wako nakala ya ushahidi wako.

Lazima uonyeshe kwamba kweli unaogopa kutendewa vibaya ikiwa utarudi katika nchi yako. Hii pia inajulikana kama “hofu ya kibinafsi.” Hapa kuna baadhi ya mifano ya maswali ambayo Mwanachama anaweza kukuuliza:

  • Baada ya kutendewa vibaya katika nchi yako, kwa nini hukuondoka mara moja?
  • Kwa nini ulipitia nchi nyingine salama ulipokuwa unaelekea Kanada (kwa mfano, Marekani), lakini hukutoa dai?
  • Kwa nini ulirudi katika nchini yako baada ya kuondoka?
  • Kwa nini ulisubiri kutoa dai baada ya kufika Kanada?

Fikiria juu ya maswali haya na majibu yako. Jitayarishe kadri uwezavyo kabla ya kusikilizwa kwako. Je, una ushahidi ambao utakusaidia kueleza ulichofanya au kutofanya? Kwa mfano, ulitumaini kwamba hali katika nchi yako ingebadilika? Je, ilikuwa vigumu kuondoka katika nchi yako?

Mifano ya ushahidi

Hapa kuna baadhi ya mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kusaidia kuonyesha kwa nini unaogopa kurudi katika nchi yako:

  • Ripoti za polisi zinazoonyesha ulitafuta usaidizi kwa polisi au uliripoti uhalifu dhidi yako
  • Ripoti za daktari za matibabu yoyote au majeraha
  • Uthibitisho kwamba ulijaribu kutoroka hatari (kama vile tikiti, risiti, hati za kusafiri)
  • Taarifa za mashahidi kwamba ulijaribu kujikinga na vitisho
  • Taarifa ulizokusanya kuhusu kutoa dai katika nchi nyingine
  • Hati zinazoonyesha kwa nini hukuweza kuondoka nchi yako mapema
  • Hati zinazoonyesha kuwa ulipata tabu kutuma madai nchini Kanada mara tu ulipowasili
  • Uthibitisho wako wa kuwasili na kuingia Kanada

Ni lazima uonyeshe kwamba wewe binafsi unakabiliwa na hatari ya kuteswa au kudhuriwa katika nchi yako. Lazima uonyeshe kuwa hii sio hatari ya jumla katika nchi yako. Kwa mfano, ikiwa kuna vurugu nyingi, lazima uonyeshe kwa nini wewe binafsi uko hatarini. Ukiweza, taja ni nani (au kikundi gani) kimekulenga, kwa nini, na unajuaje.

Lazima pia uonyeshe kuwa uko hatarini kwa sababu ya rangi yako, dini, utaifa, maoni ya kisiasa, au uanachama wako katika kikundi cha kijamii. Hii inaitwa misingi ya Mkataba. Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, muulize ni sababu zipi zinaweza kutumika kwako.

Mifano ya ushahidi

Hii hapa ni baadhi ya mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kuonyesha kuwa uko katika hatari ya kudhuriwa katika nchi yako:

  • Vidokezo vyovyote, barua, ujumbe wa simu unaoonyesha vitisho vya vurugu
  • Taarifa rasmi kutoka kwa mashahidi wakisema kwamba wewe, au watu kama wewe, mmekuwa waathirika wa ukatili
  • Picha za majeraha au aina nyingine za uharibifu
  • Picha za uporaji au uharibifu ulioona (au ulioshiriki)
  • Rekodi za matibabu
  • Ripoti za polisi kutoka kwa nchi yako
  • Ushahidi wa mitandao ya kijamii au video (ikiwa video ina mtu yeyote anayezungumza, maneno hayo lazima yaandikwe na kutafsiriwa kwa Kiingereza au Kifaransa)

Lazima uonyeshe kuwa serikali yako haiwezi au haitaki kulinda.

Ikiwa ulijaribu kupata ulinzi kutoka kwa watu wenye mamlaka katika nchi yako lakini haukuupata:

  • Eleza ni nini ulichofanya na jinsi walivyokujibu.
  • Jaribu kupata hati zinazoonyesha kwamba ulijaribu kupata usaidizi.
  • Jaribu kutafuta ripoti kutoka nchi yako zinazoonyesha kwamba mamlaka yenu haiwezi au haitaki kulinda watu kama wewe.

Iwapo hukujaribu kupata ulinzi kutoka kwa mamlaka ya nchi yako:

  • Eleza kwa nini na ujaribu kupata hati zinazo onyesha kwamba haikuwa busara kufanya hivyo.
  • Toa mifano ya kile kilichotokea kwa watu wengine ambao walijaribu kuomba msaada.

Mifano ya ushahidi

Hapa kuna baadhi ya mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ili kuonyesha kwa nini serikali yako haiwezi kukulinda:

  • Ripoti za nchi au habari zinazoonyesha ufisadi wa serikali au ukosefu wa ulinzi kutoka kwa polisi
  • Ripoti ulizotoa kwa polisi
  • Kauli kutoka kwa watu walio katika hali kama yako. (Ni vyema wakisema kuwa ni ukweli mbele ya mwanasheria au mthibitishaji wa umma. Pia waombe nakala ya kitambulisho chao.)

Lazima uonyeshe kwamba si salama au haiwezekani kwako kuishi katika sehemu yoyote ya nchi yako.

IRB-RPD inaweza kutaja jiji katika nchi yako ambapo wanafikiri unaweza kuhamia na kuishi kwa usalama. Hii inajulikana kama “sehemu mbadala ya ndani ya nchi ya kuhamia” Lazima uonyeshe kwamba:

  • huwezi kuishi huko kwa usalama, au
  • haitakuwa jambo la busara kwako kuishi huko (kwa sababu ya umri wako, jinsia, au hali, kwa mfano).

Mifano ya ushahidi

haitakuwa jambo la busara kwako kuishi huko (kwa sababu ya umri wako, jinsia, au hali, kwa mfano).

  • Hati zinazoonyesha ulijaribu kujiepusha na matatizo kwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yako.
  • Ripoti zinazoonyesha tatizo hilo liko nchi nzima. Kwa mfano, watu unaowaogopa wako kote nchini, au matendo unayoogopa yapo katika sehemu zote za nchi yako.
  • Ripoti zinazoonyesha kwa nini mtu kama wewe angeona vigumu kuishi katika eneo hilo. Kwa mfano, ripoti zinazoelezea utamaduni katika nchi yako au kuonyesha kwamba kuna matatizo makubwa katika eneo hilo.
  • Barua kutoka kwa marafiki au jamaa waliokusaidia kujificha katika sehemu mbalimbali za nchi yako.
  • Ripoti zinazoonyesha kwamba hakuna njia ya kufika katika eneo hilo, kwa sababu ya vita, maafa ya asili, au sababu nyinginezo.

IRB-RPD inaweza kukataa dai lako kwa sababu ya uhalifu. Hii inaitwa kutengwa. Hii inaweza kutokea ikiwa IRB-RPD inafikiri ume:

  • ulifanya uhalifu wa kivita,
  • ulifanya uhalifu mkubwa usio wa kisiasa nje ya Kanada, au
  • ulivunja sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Hakikisha unazungumza na wakili ikiwa IRB-RPD itakuambia kuwa watakuwa wanachunguza uhalifu kama sehemu ya dai lako la ukimbizi.

Mifano ya ushahidi

Hapa kuna baadhi ya mifano ya ushahidi unaoweza kukusanya ikiwa IRB-RPD itasema umehusika katika shughuli za uhalifu:

  • Rekodi ya mahakama ya hatia yoyote
  • Rekodi za polisi za ukweli ambao uliripotiwa kwao kwanza
  • Taarifa za mashahidi kuhusu mashtaka
  • Maoni ya kisheria kutoka kwa mwanasheria kutoka nchi yako

Ikiwa hukutoa dai la ukimbizi mara tu ulipowasili Kanada, lazima ueleze ni kwa nini ulichelewa kufanya hivyo. Unaweza kuulizwa ueleze kwa nini hukuondoka nchini kwako mapema, kutoa madai katika nchi nyingine, au kutoa dai la ukimbizi mara tu ulipowasili Kanada.

Ni muhimu kufikiria jinsi utakavyoweza kujibu maswali haya kwa sababu IRB-RPD inaweza isiamini kuwa kwa kweli unaogopa kurudi katika nchi yako ikiwa ulichelewa kutoa dai lako.

Ikiwa hukutoa dai la ukimbizi haraka, fikiria maswali yafuatayo ili ikusaidie kueleza sababu yako ya kuchelewa:.

  • Je, uliogopa kurudi katika nchi yako muda fulani baada ya kufika Kanada?
  • Je, hukujua kwamba unapaswa kutoa dai mara tu unapowasili Kanada?
  • Je, ulipata tabu kutoa dai au kupata mwakilishi wa kisheria?
  • Je, hukujua jinsi ya kutoa madai na ilikuchukua muda kujua?

Toa maelezo na ujitahidi kueleza hali hiyo au mazingira yalivyokuwa. Kuwa tayari kujibu maswali ambayo Mwanachama anaweza kuwa nayo kuhusu kuchelewa kwako wakati wa kusikilizwa kwako.

Jinsi ya Kutuma Ushahidi Wako

Mahitaji ya ushahidi

Ushahidi wako wote lazima uwe kwa lugha ya Kiingereza au Kifaransa. Ikiwa una hati katika lugha nyingine, unahitaji kuzitafsiri kwa Kiingereza au Kifaransa. Ikiwa unawasilisha video au sauti iliyorekodiwa kama ushahidi, utahitaji uandike nakala inayohadithia ya kila kinachosemwa. Nakala hii lazima pia itafsiriwe kwa Kiingereza au Kifaransa.

Kuna tarehe ya makataa ya kutuma ushahidi wako. Ushahidi wote lazima utumwe kwa IRB-RPD angalau siku 10 kabla ya kusikilizwa kwa ombi lako la mkimbizi. Hakikisha umetuma ushahidi wako kabla ya mda wa kutuma ushahidi kuisha.

Ushahidi lazima uwasilishwe katika muundo maalum. Endelea kusoma hapa chini ili ujue zaidi:

Ikiwa una mwakilishi wa kisheria

Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, atawasilisha nyaraka zako kwa niaba yako. Mpe mwakilishi wako wa kisheria ushahidi na nyaraka zako zote. Anaweza kukusaidia kuamua ni nyaraka zipi ni muhimu na ataziwasilisha kwa IRB-RPD. Hakikisha unampa muda wa kutosha.

Ikiwa huna mwakilishi wa kisheria

Ikiwa umealikwa kutumia My Case, lazima uwasilishe ushahidi wako kupitia tovuti ya My Case portal. Unaweza kutumia njia nyingine tu ikiwa utapata ruhusa kutoka kwa IRB-RPD.

Ikiwa unajiwakilisha mwenyewe na hujapokea mwaliko wa My Case, unaweza kuendelea kutuma nyaraka kwa barua pepe (inapendekezwa) au kwa posta.

Unapowasilisha ushahidi wako, kumbuka mambo muhimu yafuatayo:

  • Hakikisha hati zako zote ziko kwenye karatasi ya ukubwa wa 8.5 x 11. Hati zilizoandikwa lazima ziwe na herufi zilizo na ukubwa wa angalau 12.
  • Weka hati zako pamoja na uziandike namba kutoka ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho.
  • Tengeza ukurasa wa jalada wenye jina na anwani yako, tarehe, nambari yako ya faili ya IRB-RPD, orodha ya hati zako zote, na nambari zao za ukurasa.
  • Tengeneza nakala za hati zako zote. Weka nakala ya asili
  • Ikiwa unawasilisha hati zako kwa kutumia barua pepe hakikisha kuwa ziko katika umbizo la PDF

Tuma nakala moja ya kifurushi chako cha hati kwa IRB-RPD katika eneo lako. Eneo ulilopo linategemea na mahali unapoishi. Ukihamia eneo lingine, unaweza kuomba dai lako lihamishwe hadi eneo hilo:

Ikiwa unaishi British Columbia, Alberta, Saskatchewan, Manitoba, Yukon, Northwest Territories.

Barua pepe

  • RPDWestern-SPRouest@irb-cisr.gc.ca
    • Fuata maelekezo haya kwa makini: Lazima utume nyaraka zako kama viambatisho katika mfumo wa PDF. Faili za PDF hazipaswi kuzidi 20MB. Katika mstari wa mada, weka nambari yako ya UCI (na nambari yako ya IRB-RPD na tarehe ya usikilizaji ikiwa unayo) na eleza kuwa nyaraka za ushahidi zimeambatishwa. Usiandike chochote katika mwili wa barua pepe.

Barua

Ikiwa huwezi kutumia njia nyingine zozote, unaweza kutumia huduma ya posta au courier. Hifadhi nyaraka zako za asili na risiti. Hakikisha unatuma kifurushi chako mapema ili kifike kwa wakati.

  • IRB-RPD, Minto Place, Canada Building 344 Slater Street, Ghorofa ya 12 Ottawa, Ontario Canada, K1A 0K1I

    Ana kwa ana

    • IRB–RPD, 300 West Georgia Street, Suite 1600 Vancouver, BC V6B 6C9
      • Ikiwa unaishi Vancouver unaweza kuwasilisha hati zako mwenyewe katika ofisi ya IRB.

    Ikiwa unaishi Ontario (isipokuwa Ottawa na Kingston)

    Barua pepe

    • RPDCentral-SPRcentre@irb-cisr.gc.ca ​​
      • Fuata maagizo haya kwa uangalifu: Lazima utume hati zako katika umbizo la PDF. Faili za PDF haziwezi kuwa na ukubwa uliozidi MB 20. Katika mstari wa mada, weka nambari yako ya UCI (na nambari yako ya IRB-RPD na tarehe ya kusikilizwa ikiwa unayo) pamoja na kutaja ni hati gani unazozituma. Usiandike chochote kwenye mwili wa barua pepe.

    Barua

    Ikiwa huwezi kutumia njia nyingine zozote, unaweza kutumia huduma ya posta au courier. Hifadhi nyaraka zako za asili na risiti. Hakikisha unatuma kifurushi chako mapema ili kifike kwa wakati.

    • IRB-RPD, Minto Place, Canada Building 344 Slater Street, Ghorofa ya 12 Ottawa, Ontario Canada, K1A 0K1

      Ana kwa ana

      • 25 St. Clair Avenue East, Suite 400, Toronto, Ontario M4T 0A8
        • Ikiwa unaishi Toronto unaweza kuwasilisha hati zako mwenyewe katika ofisi ya IRB.

      Ikiwa unaishi Quebec, New Brunswick, Nova Scotia, Prince Edward Island, Newfoundland, Nunavut, Kingston (Ontario), Ottawa (Ontario)

      Barua pepe

      • RPDEastern-SPRest@irb-cisr.gc.ca
        • Fuata maagizo haya kwa uangalifu: Lazima utume hati zako katika umbizo la PDF. Faili za PDF haziwezi kuwa na ukubwa uliozidi MB 20. Katika mstari wa mada, weka nambari yako ya UCI (na nambari yako ya IRB-RPD na tarehe ya kusikilizwa ikiwa unayo) pamoja na kutaja ni hati gani unazozituma. Usiandike chochote kwenye mwili wa barua pepe.

      Barua

      Ikiwa huwezi kutumia njia nyingine zozote, unaweza kutumia huduma ya posta au courier. Hifadhi nyaraka zako za asili na risiti. Hakikisha unatuma kifurushi chako mapema ili kifike kwa wakati.

      • IRB-RPD, Minto Place, Canada Building 344 Slater Street, Ghorofa ya 12 Ottawa, Ontario Canada, K1A 0K1

        Ana kwa ana

        • Guy-Favreau Complex, 200 René-Lévesque Blvd. West, East Tower, Room 102, Montréal, Quebec H2Z 1X4
          • Ikiwa unaishi Montreal unaweza kuwasilisha hati zako mwenyewe katika ofisi ya IRB.

        Je, Wadai Wote Wana Usikilizaji wa Kesi?

        IRB-RPD huamua baadhi ya madai ya ukimbizi bila kusikilizwa, au kwa kutumia kusikilizwa kwa muda mfupi tu. Hii inaitwa Mchakato wa Madai Magumu Kiasi. IRB-RPD inaweza kukutambulisha kwa mchakato huu ikiwa:

        • madai kama yako au kutoka nchi yako kwa kawaida huidhinishwa,
        • ni rahisi kujua utambulisho wako,
        • ushahidi kuhusu hatari yako ni wazi na moja kwa moja, na
        • hakuna uwezekano kwamba suala lolote gumu litatokea.

        IRB-RPD inaweza kuamua kwamba:

        • kusikilizwa hakuhitajiki ili kuidhinisha dai lako la ukimbizi, au
        • kusikilizwa kwa muda mfupi tu kunahitajika ili kuamua dai lako.

        Madai yanayoamuliwa bila kusikilizwa

        Iwapo IRB-RPD inafikiri dai lako linaweza kuamuliwa bila kusikilizwa, itakutumia notisi kwamba dai lako liko kwenye Mchakato wa Kukagua Faili (FRP) . Katika notisi hii, IRB-RPD itakuuliza wewe au mwakilishi wako kutuma ushahidi mwingine wowote ulio nao. Lazima pia utie sahihi fomu ya uthibitisho na uirejeshe pamoja na ushahidi wako.

        Baada ya IRB-RPD kupata fomu yako watakagua kesi yako. Watakuwa ama:

        • Kubali dai lako bila kusikilizwa. Wewe au mwakilishi wako wa kisheria mtapata Notisi ya Uamuzi ikisema dai lako limekubaliwa, au
        • Amua kusikilizwa au kusikilizwa kwa muda mfupi kunahitajika ili kufanya uamuzi juu ya dai lako. Utapokea barua yenye maelezo kuhusu kusikilizwa kwako.

        Madai ambayo yanaweza kusikilizwa kwa muda mfupi

        Usikilizaji wa kawaida huchukua masaa 3-4, wakati kusikia kwa muda mfupi huchukua masaa 1-2 tu. IRB-RPD inaweza kukupa usikilizaji mfupi ikiwa:

        • madai mengi kutoka katika nchi yako aidha yanakubaliwa au HAYAKUBALIWI (kumaanisha kuwa yana viwango vya juu sana vya kukubalika au vya chini sana),
        • dai lako lina suala moja au mbili muhimu la kujadili, na
        • hakuna masuala magumu katika dai lako.

        Iwapo IRB-RPD inafikiri dai lako linaweza kuamuliwa kwa kusikilizwa kwa muda mfupi, itakutumia Notisi Maalum ya Kutokea. Ikiwa unafikiri kusikia kwako kunahitaji zaidi ya saa mbili, omba kusikilizwa kwa muda mrefu mara moja na ueleze ni kwa nini. Iwapo IRB-RPD itakubali, itakusikiliza kwa muda mrefu siku hiyo hiyo, au tarehe ya baadaye.

        Madai ambayo hayawezi kusikilizwa kwa muda mfupi

        Dai lako halitaweza kuamuliwa kwa kusikilizwa kwa muda mfupi ikiwa:

        • Wakili wa Waziri anataka kuingilia kati kupinga dai lako kwenye kikao chako.
        • IRB-RPD imemwambia Waziri kunaweza kuwa na suala zito na dai lako.

        Jitayarishe kwa ajili ya Siku Yako ya Kusikilizwa

        Kuna njia nyingi muhimu za kujiandaa kwa ajili ya siku yako ya kusikilizwa. Mkutano wako wa kusikilizwa ni fursa yako ya kukutana na Mwanachama wa IRB-RPD na uweze kujibu maswali kuhusu dai lako. Ukijitayarisha vizuri, utaweza kujibu mswali vizuri na utakuwa unajiamini.

        Fanya mazoezi ya kujibu maswali

        Mojawapo ya mbinu za kujiandaa kwa ajili ya kusikilizwa kwa dai lako ni kufanya mazoezi ya kujibu maswali ambayo Mwanachama anaweza kukuuliza. Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, mwambie achukue muda akufanyishe mazeozi ya kujibu maswali kabla ya kusikilizwa kwako. Muulize ni maswali gani unaweza kuulizwa, na ni jinsi gani unafaa uyajibu maswali hayo. Jinsi unavyozidi kufanya mazoezi ya kujibu maswali, itakuwa ni bora zaidi kwako!

        Ikiwa huna mwakilishi wa kisheria, unaweza kukagua fomu yako ya BOC, hadithi yako, pamoja na ushahidi wowote uliowasilisha. Fikiria ni jinsi ungejibu maswali kulingana na maelezo yaliyoko kwenye hati zako.

        Fanya mazoezi ya kujibu maswali kuhusu:

        • Kasoro yoyote iliyoko kwenye hadithi yako au hati zako
        • sehemu mbalimbali za hadithi yako
        • kwa nini unadhani utakuwa hatarini ukirudi katika nchi yako
        • kama unaweza kuishi kwa usalama katika sehemu nyingine ya nchi yako
        • maamuzi yoyote uliyoyafanya, kama mfano: kwa nini uliamua kuondoka nchi yako wakati ulipoondoka na sio mapema, au kwa nini ulisubiri kabla ya kutuma dai la ukimbizi nchini Kanada.

        Unaweza pia kufanya mazoezi ya kujibu maswali ambayo huyaelewi au huyajui. Mwanachama akikuuliza swali ambalo hulielewi, usijaribu kulijibu. Mwambie Mwanachama kwamba humuelewi na umwambie akuulize kwa njia nyingine. Usiwahi kutunga jibu la uongo. Ikiwa hujui kitu, au huna uhakika, sema hivyo.

        Leta hati zako zote

        Utahitaji kuwa na fomu zote pamoja na ushahidi wowote ulioutuma kwa IRB-RPD wakati wa mkutano wako wa kusikilizwa. Hakikisha hati zako zote ziko sehemu moja ili uweze kuzileta kwa urahisi. Unapaswa kuleta:

        • Fomu ya BOC
        • Hadithi yako au simulizi yako
        • Fomu zako za uhamiaji
        • ushahidi
        • barua ya Kukuarifu Uende

        Mwanachama huwa atakuambia usisome kutoka kwenye hati zako wakati wa kujibu maswali. Lakini bado unahitajika kuwa nazo hati zako endapo Mwanachama atakuambia uziangalie. Kwa mfano, mwanzoni mwa kusikilizwa kwako, Mwanachama atakuuliza ukague saini iliyoko kwenye fomu yako ya BOC. Mwanachama pia anaweza kukuambia uangalie sehemu maalum ya hati zako ikiwa ana maswali kuhusu sehemu hiyo.

        Hudhuria Ziara ya Kujitayarisha Kusikilizwa

        Njia moja ya kujiandaa kwa ajili ya kusikilizwa kwako ni kuhudhuria Ziara ya Kujitayarisha Kusikizwa. Ziara za Kujitayarisha Kusikizwa ni za bure na huwa zinafanywa mtandaoni. Utajifunza jinsi kikao chako cha kusikilizwa kitakavyokuwa na jinsi unavyoweza kujiandaa. Utasikia kutoka kwa mfanyakazi wa IRB-RPD, na utakuwa na nafasi ya kuuliza maswali yoyote uliyo nayo kuhusu mkutano wa kusikilizwa.

        Haya ni baadhi ya mambo utakayojifunza wakati wa Ziara ya Kujitayarisha Kusikizwa:

        • Jinsi ya kuomba upate mkalimani wakati wa kikao cha kusikiliza ombi lako
        • Ni aina gani za ushahidi unaweza kukusanya utakaosaidia dai lako
        • Baadhi ya masuala ya kisheria ambayo yanaweza kujadiliwa kwenye kikao chako
        • Jinsi ya kutuma ushahidi kwa IRB-RPD
        • Jinsi mkutano wa kusikizwa unavyofanywa mtandaoni
        • Nani atahudhuria mkutano wako wa kusikizwa
        • Utajuaje kama dai lako limekubaliwa au limekataliwa

        Bofya hapa ili ujiandikishe kwenye Ziara ya Kujitayarisha Kusikizwa.

        Panga ni mahali gani utafanya mkutano wako wa kusikilizwa

        Mikutano ya kusikizwa mara nyingi hufanywa mtandaoni na si katika ofisi ya IRB-RPD. Utagundua kama usikilizaji wako ni wa mtandaoni au wa ana kwa ana utakapopokea barua ya Kukuarifu uende mbele ya IRB-RPD.

        Ikiwa mkutano wako wa kusikizwa utafanywa kwenye mtandao, utahitaji kupanga ni wapi na jinsi gani utahudhuria mkutano huo. Kuna mahitaji fulani ya kiteknolojia ambayo ni lazima uyatimize ili usikilizwe mtandaoni. Na pia ni lazima upate sehemu ya faragha. Soma zaidi kuhusu mahitaji hayo hapa.

        Ikiwa una mwakilishi wa kisheria, muulize kama utafanya mkutano wako wa kusikilizwa kwenye ofisi yake. Ikiwa huna mwakilishi wa kisheria, fikiria ikiwa unaweza kuufanya mkutano wako wa mtandaoni nyumbani. Je, una mtandao wa kihakika? Una kompyuta au kifaa chenye kamera ya video? Una chumba cha faragha kilicho na utulivu? Ikiwa huna vitu hivi, hapa kuna njia nyingine:

        • Ikiwa una wakala wa kusaidia wageni ambaye amekuwa akikusaidia, muulize kama unaweza kuja ofisini kwao kwa ajili ya kufanya mkutano wako wa kusikilizwa.
        • Waandikie IRB-RPD uwaulize kama unaweza kutumia kompyuta yao na chumba kwenye ofisi yao ili uweze kuhudhururia mkutano wako wa kusikilizwa mtandaoni.

        Iwapo unafikiri kuwa usikilizaji wa ana kwa ana utakuwa bora zaidi kwako, unaweza kuwaandikia IRB-RPD ili kuwaomba wabadilishe mkutano wako usifanywe mtandaoni. Eleza sababu zako. Soma zaidi kuhusu jinsi ya kubadilisha mkutano wako ufanywe ana kwa ana kwenye tovuti ya IRB-RPD.

        Fanya mipango ujue watoto wako watakuwa wapi waki wa kusikizwa

        Ikiwa una watoto walio chini ya umri wa miaka 18 si lazima wahudhurie kwenye kikao cha kusikilizwa dai lako, isipokuwa ikiwa IRB-RPD itaandika barua kuwaambia wahudhurie.

        Chagua mahali ambapo watoto wako watakuwa wakati wa kusikilizwa kwa dai lako. Ikiwa kesi yako inasikizwa mtandaoni na utakuwa nyumbani, jaribu kuhakikisha kuwa watoto wako hawako karibu na wewe. Mkutano wa kusikiza dai lako ni muhimu sana, na itasaidia kuhakikisha kuwa hakuna usumbufu wowote. Inaweza kuwa unazungumzia matukio ambayo yanahuzunisha sana au ni magumu. Kwa sababu hii, huenda ukawa hutaki watoto wako wayasikie. Ikiwezekana, waambie watoto wako waende shule au wakae na jamaa au rafiki, au umlipe mtu awaangalie.

        Ikiwa huwezi kupata mtu wa kuwaangalia watoto wako, au una mtoto mchanga sana, mwambie Mwanachama mwanzoni mwa mkutano.

        Badilisha tarehe na wakati wa mkutano wa kusikilizwa

        Unaweza kuomba ubadilishiwe tarehe au saa ya kusikilizwa ikiwa una dharura au ugonjwa. Huwezi kuomba kubadilisha mkutano wako wa kusikizwa kwa sababu nyingine yoyote.

        Ikiwa una dharura au ugonjwa, wewe au mwakilishi wako wa kisheria ni lazima:

        • Muwajulishe IRB-RPD kwa kuwaandikia barua pepe au kuwatumia faksi angalau siku tatu za kazi kabla ya mkutano wako wa kusikilizwa.
        • Pendekeza tarehe na nyakati nyingine tatu za kusikilizwa kwako. Tarehe hizi mpya ni lazima ziwe ndani ya siku kumi za kazi kutoka tarehe yako ya awali ya kusikilizwa.
        • Tuma cheti cha matibabu kutoka kwa daktari wako ikiwa sababu yako ya kubadilisha tarehe ya kusikizwa ni ugonjwa. Ikiwa huwezi kupata cheti cha matibabu, lazima uandike barua inayoelezea kwa nini.

        Siku ya kusikizwa

        Soma barua ya Taarifa ya Kutokea kwa makini. Itakuambia ni saa ngapi mkutano wako wa kusikzwa utakuwa, na ikiwa mkutano wako ni wa ana kwa ana au ni wa mtandaoni. Utaombwa ufike dakika 15 kabla ya muda wa kuanza mkutano wako wa kusikilizwa.

        Ikiwa unahitaji kusafiri kuenda sehemu ya kusikilizwa, kama vile ofisi ya wakili wako au ofisi ya IRB-RPD, hakikisha kuwa umepanga safari yako na uhakikishe kuwa utafika kwa wakati unaofaa au ufike mapema.

        Hakikisha ulialala vizuri kabla ya kuhudhuria mkutano wa kusikizwa, na uwe umekula vizuri. Kumbuka, unaweza kuomba upewe mda wa mapumziko wakati mkutano unaendelea ikiwa utahitaji kupumzika.